UADILIFU NI MSINGI WA USALAMA WA TANZANIA: NAIBU WAZIRI SANGU

0

Septemba 5, 2024

“Tuwawajibishe au kuachana na watumishi wasiokuwa waadilifu kwa kuwa sisi ndio tunaotakiwa kusimamia uadilifu lakini miongoni mwetu tunakuwa na watu wasiokuwa waadilifu”

Maneno hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu wakati akiongea na viongozi na watumishi wa TAKUKURU makao makuu Dodoma.

Amewakumbusha Viongozi na watumishi hao kuwa suala la uadilifu limeandikwa hata katika vitabu vya dini zote ambapo likizingatiwa kwa usahihi amani na utulivu hutamalaki miongoni mwa wananchi.

Alisema, TAKUKURU ni taasisi muhimu na nyeti katika taifa la Tanzania na msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lengo ikiwa ni kuzuia na kupambana na rushwa katika jamii. Hivyo, Viongozi na watumishi wote wa Umma wakiongozwa na TAKUKURU hawanabudi kumuunga mkono Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapambano hayo.

Mhe. Sangu ametoa rai kwa TAKUKURU kuangalia kwa kwa makini eneo la Ununuzi wa Umma ambapo zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inaelekezwa katika eneo hilo. Hivyo, eneo hilo lazima litazamwe na kupewa kipaumbele ili kuziba mianya ya rushwa.

Aliongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo Tanzania nzima, hivyo ameielekeza TAKUKURU kufuatilia na kusimamia vyema miradi hiyo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa mujibu wa mikataba.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu Bw. Mululi Majula Mahendeka amesema TAKUKURU ni muhimu kwa usalama wa nchi hasa katika kuzuia na kupambana na rushwa.

“Rushwa ikishamili na usalama wa nchi unateteleka kwa kuwa wananchi wanakosa imani na Serikali yao, hivyo ametoa wito kwa watumishi hao kufanya kazi kwa juhudu na maarifa ili Serikali iendelee kuiaminika kwa umma” alisisitiza Bw. Mahendeka.

Alibainisha kuwa, usiri na utengano sambamba ni jambo la msingi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na mambo hayo yasipozingatiwa na kutiliwa mkazo yanaweza kubomoa msingi wa umoja wa Taifa ambao uliwekwa na unaendelea kusimamiwa vyema na Viongozi wetu wakuu.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Chalamila alimuahidi Mhe. Sangu kupata ushirikiano wa dhati kutoka kwa Viongozi na Watumishi wa TAKUKURU ili kutekeleza majukumu aliyopewa kwa ufanisi.

Pia, alimuomba Mhe. Sangu kufikisha salaamu za shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *