WAZIRI MAVUNDE AGEUKA MBOGO; ATAKA MRADI WA DHAHABU MAGAMBAZI UZALISHAJI MKUBWA
Waziri wa Madini, Mh.Anthony Mavunde amebainisha kuwa kusuasua kuanza kwa mradi wa uchimbaji dhahabu wa Magambazi uliopo Kijiji cha Nyasa Wilayani Handeni kunapelekea kuikosesha Serikali mapato na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi huo.
Ameyasema hayo leo tarehe 23 Agosti, 2024 Jijini Tanga alipokutana wawakilishi wa wananchi wa Handeni na Kampuni za CANACO Tanzania Ltd. na PPM Mining ambazo zinahusika na utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa mujibu wa taarifa za utafiti wa madini uliofanyika katika eneo la mradi huu, zinaonesha kuna zaidi ya wakia za dhahabu 700,000 na kwa hivi sasa mnasema mnazalisha dhahabu kiasi cha chini ya gramu 50, huku ni kuwanyima Watanzania haki ya kunufaika na rasilimali walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu”
“Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha tunahamasisha na kuongeza shughuli za uchimbaji ili kuongeza mapato. Hivyo, ni dhahiri kwamba kunapokuwa na hali kama hii ya kusuasua kwa mradi ambao ulipaswa kuwa umefika mbali katika hatua za uwekezaji na uzalishaji, ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali, na kwa kweli sisi tuliopewa dhamana hatuwezi kukubali.
Dhamira njema ya Serikali kwa wawekezaji ndiyo iliyotusukuma Wizara ya Madini kuunda Timu Maalum kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika mradi huu ili ije itushauri namna bora ya kuufanya mradi huu kuanza uzalishaji kama tulivyokusudia.
Vilevile, baada ya kuwapa nafasi na kuwasikiliza wawakilishi wa Kampuni zote mbili za Canaco na PPM ambao ndiyo wahusika wakuu wa utekelezaji wa mradi wa Magambazi, Waziri Mavunde aliziagiza Kampuni hizo kwenda kukaa pamoja ndani ya muda mfupi na kukubaliana kwenye masuala yote baina yao yanayopelekea mradi huo kusuasua ili uanze kuzalisha kwa tija.
Pia, Mhe. Mavunde alisisitiza kwamba Sheria ya Madini Sura ya 123 inaeleza wazi masharti na wajibu wa mtu yeyote au Kampuni itayokuwa ikimiliki leseni ya madini, na kumtaka mmiliki wa leseni ya uchimbaji kwenye mradi wa Magambazi kuzingatia masharti hayo ili kuchochea maendeleo ya wananchi wa Handeni na Taifa kwa ujumla.
Kutokana na muda wa kuhuisha leseni hiyo kufika, Serikali kupitia Tume ya Madini imetoa notisi kwa mmiliki wa leseni na kuweka matakwa ya sheria yanayotakiwa kufanyiwa kazi kupitia barua ya notisi ya tarehe 12 Agosti, 2024 yawe yamekamilika ifikapo Septemba 1 mwaka 2024.
Akitoa maelezo ya utangulizi katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba alieleza kwamba tayari amekwishafanya vikao kadha wa kadha na wawekezaji hao kwa lengo la kuhakikisha mgodi huo unaanza uzalishaji kwa tija na kusisitiza kuwa wananchi na viongozi wa Handeni wana matumaini makubwa na mgodi huo kwenye kusukuma maendeleo ya Handeni.
Awali, akieleza umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Handeni, Mbunge wa Jimbo la Handeni, Mheshimiwa Mhandisi John Sallu aliishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za kutaka kuanza kwa mradi huo na kueleza matumaini makubwa ya wananchi wa Handeni kuwa tayari kupokea kuanza kwa uzalishaji katika mgodi huo wa dhahabu wa Magambazi.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili msomi Mheshimiwa Albert Msando alikiri kukutana na wawekezaji hao mara kadhaa, na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuendelea kusimamia kuanza uzalishaji kwa mradi huo ili uchochee maendeleo ya wananchi wa Wilaya yake.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Balozi Batilda Burhani alibainisha kwamba pamoja na uwepo wa utajiri wa rasilimali nyingi katika Wilaya ya Handeni, bado wananchi wake wamekua wakiishi maisha duni na kusisitiza kuwa kuanza kwa miradi kama huo wa Magambazi kutakwenda kuchochea maendeleo ya Handeni na kuinua vipato vya wananchi.