“FANYENI UTAFITI WA MISHAHARA SERIKALINI” – SANGU
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka viongozi wa Idara zote katika ofisi yake zinazohusika na uchakataji wa mishahara, kufanya utafiti wa kina kwenye taasisi za umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ili mtumishi wa umma alipwe mshahara kutokana na ufanisi wa kazi.
Mhe. Sangu ameyasema hayo Agosti13, 2024 wakati alipokuwa akifuatilia mawasilisho mbalimbali ya majukumu ya Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu, Idara ya Uendelezaji Rasimaliwatu, Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma na Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ikiwa ni sehemu ya kujifunza kuhusu majukumu ya Ofisi yake.
“Fanyeni utafiti wa mishahara Serikalini, kuna baadhi ya taasisi zilianzishwa na Serikali kwa nia njema ili kuboresha utoaji wa huduma na zikapewa mitaji na kufanya vizuri kwa muda mfupi na sasa hakuna wanachokizalisha lakini wanalipwa mishahara mikubwa inayoiongezea Serikali gharama za uendeshaji” alisema Mhe. Sangu.
Vile vile, amesisitiza Idara ya uendelezaji Rasilimaliwatu kufanya ufuatiliaji kwa Wizara na Taasisi za Umma ili kujiridhisha kama mwongozo wa mafunzo kwa watumishi wa umma unazingatiwa ipasavyo na kuzielekeza Idara hizo kufanya utafiti kwa taasisi za umma ili kubaini taasisi zenye mwenendo huo na matokeo ya utafiti yawasilishwe kwenye mamlaka yakiambatana na mapendekezo kwa hatua zaidi.
Watumishi wanakaa ofisini bila kupewa mafunzo ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao, hivyo kushindwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu hawana ujuzi au ujuzi walionao umepitwa na wakati amesema Mhe. Sangu.
Hali kadhalika, ameongeza kuwa taaratibu za kufanya uchunguzi (vetting) kwa watumishi wanaotakiwa kushika wadhifa fulani ufanyike kwa haraka kwa kuwa kumpa nafasi au kumkaimisha mtumishi nafasi ya uongozi kwa muda mrefu na ikabainika kuwa hana sifa anaweza kuiweka Serikali kwenye matatizo.
Amepongeza kwa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kwa kupata suluhu ya uchakataji wa mishahara kwa kutumia mfumo wa e-Watumishi na sasa mishahara inachakatwa ndani ya dakika 30 hadi saa moja tu badala ya siku 14 za hapo awali.
Mhe. Sangu ameendelea na siku ya pili ya ratiba yake ya kujifunza kuhusu majukumu ya idara mbalimbali zilizopo katika ofisi yake yanayofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mtumba Jijini Dodoma