MGODI WA GGM WAANZA KUTUMIA UMEME WA GRIDI BADALA YA MAFUTA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) chenye uwezo wa megawati 34 ambacho sasa kinawezesha GGML kuanza kutumia umeme wa gridi kwa matumizi yake badala ya mafuta na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
Baada ya kuzindua kituo hicho tarehe 13 Agosti 2024 wilayani Geita mkoani Geita, Dkt.Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni alama halisi ya umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Sekta Binafsi kwani mradi huo umehusisha ujenzi wa laini ya umeme ya kV 33 ambayo imejengwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi bilioni 8.04 huku GGML ikijenga kituo cha kupoza umeme kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.
Amesema GGM ilikuwa inatumia shilingi bilioni 130 kwa mwezi kama gharama za uendeshaji na kwenye umeme wa mafuta ilikuwa inatumia shilingi bilioni 13.4 kila mwezi na kuathiri mapato yake kwa Serikali, hivyo kuanza kazi kwa kituo hicho kunapunguza gharama za uendeshaji kwa mgodi na kupelekea Serikali kuongeza mapato yake, kuongeza ajira na pia GGM kuweza kutanua shughuli zake.
Dkt.Biteko ameipongeza kampuni hiyo kwa kuanza kutumia umeme wa gridi ambao unapunguza gharama za uendeshaji ambapo ametoa angalizo kuwa, kupungua kwa gharama hizo kuguse pia watumishi kwa kuboresha maslahi yao.
Ameeleza kuwa, umeme mwingi unaozalishwa kwa sasa unatoa uhakika wa kwenda kwa wananchi na walaji wakubwa kama GGM na kuweka mkazo kuwa, hayo ni matokeo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuijali sekta binafsi.
Vilevile, ameipongeza GGM kwa kuzipa kipaumbele kampuni za kizawa katika kutoa huduma kwenye mgodi huo na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kuhakikisha kampuni za ndani zinapewa kipaumbele kwenye miradi mbalimbali.
Dkt. Biteko amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na Taasisi nyingine za Serikali kujali sekta binafsi kutokana na manufaa yake ikiwemo kuwa walipakodi wakubwa na kuongeza ajira nchini.
Pia, amewashukuru watangulizi wake katika Sekta ya Nishati, Dkt. Medard Kalemani na January Makamba ambao katika kipindi chao wakihudumu kama Mawaziri wa Nishati waliusimamia mradi huo ipasavyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema hali ya umeme nchini kwa ujumla ni nzuri huku uzalishaji ukikidhi mahitaji na ziada kidogo.
Kuhusu usambazaji umeme mkoani Geita amesema kuwa Mkoa una Vijiji 486 na kati ya hivyo vijiji 483 vina umeme sawa na asilimia 99.38.
Ameongeza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vitongojini mkoani Geita inaendelea ambapo kati ya vitongoji 2,197, vitongoji takriban 1000 tayari vina umeme.
Ameongeza kuwa, Mkoa wa Geita umetengewa Shilingi bilioni 8.5 kwa ajili ya kupeleka umeme maeneo ya migodi na viwanda na utekelezaji umefikia asilimia 41.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ambayo yamepelekea wawekezaji kufanya kazi na kuletea nchi faida akitolea mfano kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu GGM imezalisha tani 51 za dhahabu ambayo ni mafanikio makubwa yanayochangia ukuaji wa pato la Taifa.
Amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha umeme kufika pia kwenye migodi ya Wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu wachimbaji wadogo 19 wamepelekewa umeme kwenye migodi yao na kuwezesha uzalishaji wa kilo za dhahabu takriban 11,000.
Wabunge mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Rais Samia pamoja na uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kutekeleza mradi huo ambao una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi na mgodi wenyewe.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha.Abubakari Issa amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho kutaiwezesha GGML kuanza kutumia umeme wa gridi kwenye matumizi yake pamoja na kuongeza mapato ya TANESCO ambapo inategemewa yataongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni 2 hadi 3 kwa mwezi.
Makamu wa Rais wa kampuni ya Anglo Gold Ashanti-Tanzania anayeshughulikia Miradi Endelevu, Simon Shayo ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na miundombinu madhubuti ya umeme inayowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi.
Amesema mradi huo ni muhimu kwa GGM kwani unawawezesha kupata umeme wa gridi na kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta ambapo gharama zitapungua kwa asilimia 92.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo ni Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Bunge, Wabunge kutoka Mkoa wa Geita, Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na GGM.