WHI MKUTANO WA MWAKA NI AGOSTI 10 UKWASI 27B

0

Na.Mwandishi Wetu

Taasisi ya Watumishi Housing Investiment (WHI) kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Faida (Faida Fund) katika kipindi cha mwaka mmoja wamefanikiwa kukuza thamani ya mfuko kutoka shilingi bilioni 12 hadi kufikia bilioni 27, huku wakitarajia kufanya mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka Agosti 10, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umelenga kutoa fursa kwa wawekezaji wa mfuko kupokea na kujadili maendeleo, mipango pamoja na taarifa ya fedha kwa kipindi cha mwaka mmoja unaoishia Juni 30, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 6, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi mtendaji wa WHI Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu mfuko umepiga hatua kubwa kwani thamani ya vipande viliuzwa kwa shilingi 100 na sasa vinauzwa kwa shilingi 117 sawa na ukuaji wa asilimia 17.

Dkt. Msemwa amesema kuwa mafanikio hayo yametokana mazingizira mazuri ya kufanya biashara nchini ikiwemo kutoa fursa kwa wawekezaji wadogo kuwekeza kuanzia sh. 10,000.

“Pia tumeweza kubuni mfumo wa kipekee ambao unauwezo wa kuchaka fedha unaotumiwa na faida Fund, mfumo huu unawezesha mwekezaji kuwekeza na kupata faida pamoja na kuchukua fedha zao bila kulazimika kujaza fomu au kufika ofisini” amesema Dkt. Msemwa.

Amesema kuwa mfumo huo ni wa kwanza kutumika nchini ambapo ufanisi wake unatoa fursa kwa mwekezaji kuwekeza kwa kutumia simu pamoja na kuuza vipande bila kujaza fomu yoyote.

“Katika kipindi cha muda mfupi mfuko wa Faida Fund umeweka misingi imara utakaoweza kuziba ombwe la wawekezaji wadogo la kushindwa kushiiriki kwenye masoko ya uwekezaji wa fedha” amesema Dkt. Msemwa.

Amefafanua kuwa faida Fund ndio mfuko pekee wa uwekezaji unatumia mfumo wa malipo ya serikali (GEPG) na kuwa na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo mwekezaji anaweza kujaza fomu au kuchota faida mtandaoni bila kufika ofisini.

Faida Fund ni mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaosimamiwa na WHI ambao unatoa fursa ya uwekezaji kwa watanzania, vikundi, makampuni na taasisi kuwekeza kwa pamoja na kupata faida shindani kupitia ukuaji wa mitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *