GST YABAINISHA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI ZILIZOPO KANDA YA KATI
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imebanisha Fursa za Uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini Kanda ya Kati inayojumuisha Mikoa ya Dodoma na Singida ambayo wananchi wanaweza kufaidika nayo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Bw. Maswi Solomon wakati akiwasilisha mada kwenye Kongamano la Uwekezaji katika Maonesho ya Nanenane 2024 yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.
Akizungumza katika Kongamano hilo Maswi amesema Kanda ya Kati inajumuisha mikoa ya Singida na Dodomba ambayo imebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini hasa Mkoa wa Dodoma na hii ni kutokana na Mkoa huo kupitiwa na mabadiliko ya kijiolojia takribani matano (5) katika vipindi kadhaa vya umri tofauti wa kijiolojia na hivyo kila badiliko la kijiolojia kuambatana na madini aina fulani kulingana na kichocheo cha wakati husika kama Jotoardhi na mgandamizo (pressure & temperature).
Baadhi ya madini hayo ni Dhahabu, Urani, Magadi, Chuma, Chumvi, Magnesite, Vito, Jasi, Helium, Lithium, Shaba, Chrysoprase, Nikeli.
Adha, Maswi ametaja madini mengine yapatikanayo Kanda ya Kati ni pamoja na Feldspar, Quartz, Mawe ya Chokaa, Moonstone, Asbestos, Kyanite, Dolomite,Yoderite, Almasi, Pozzolana, Zircon, Bentonite na Amthyst.
Pia, Maswi amesema Wizara ya Madini imekuja na dhana ya “Vision 2030 Madini ni Maisha na Utajiri” ambayo inasaidia kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingi za Uchumi na kijamii ikiwemo Sekta ya Kilimo, Maji, Utalii, Miundombinu na Nishati kwa kufanya tafiti na kuibua maeneo yenye miamba inayohifadhi nishati kama jotoridi, maji kwa ajili ya kilimo, mifungo na matumizi ya binadamu. Hii ni pamoja na kutumia chemchemu za majimoto zilizo katika Mikoa ya Singida na Dodoma katika matumizi ya moja kwa moja (Direct uses) kama ukuzaji wa mazao, ufugaji wa kuku wa kisasa, mabwawa ya kuogelea, ufugaji wa samaki, kilimo cha kijani n.k ili kujipatia kipato.
Pia, kutumia baadhi ya madini maalum na migodi ya kisasa ya uchimbaji mfano mgodi wa dhahabu wa Shanta kama vivutio vya utalii wa jiolojia na hii iende sambamba na kutumia maeneo yenye maumbo ya asili ya kijiolojia kama vivutio vya utalii wa jiolojia kama Mapango na Michoro ya Kolo- Kondoa, Bonde la Bahi n.k.
Sambamba na hayo, Maswi ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini, Kilimo, Utalii, Maji, Nishati na Miundombinu kuitumia GST kwa ajili ya tafiti na uchunguzi wa miamba na udongo kwa maendeleo ya Taifa.
Kongamano hilo, limeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ambapo Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, Wakuu wa Wilaya za Dodoma na Singida pamoja na wadau mbalimbali wameshiriki.