KUWENI NA UTHUBUTU, TUMIENI FURSA ZA SERIKALI
Vijana wametakiwa kuwa na uthubutu na kubuni Biashara mbalimbali ili waweze kutimiza malengo na kuondokana na Changamoto ya ukosefu wa Ajira.
Wito huo umetolewa Leo Julai 27, 2024 Jijini Dodoma na Katibu Tawala Msaidizi Biashara, Viwanda na Uwekezaji Mkoa wa Dodoma Bi. Mwajabu Nyamkomora Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule katika Uzinduzi wa Kituo cha kutengeneza Juisi cha Vio Juice.
Amempongeza Mkurugenzi wa Vio Juice Bi. Vaileth kwa Ubunifu wake na kujituma kiasi ambacho ameisaidia Serikali katika suala la Ajira kwani kupitia Kituo hicho atakwenda kuajiri watanzania mbalimbali.
“Ulikuwa na uthubutu na Ujasiri wa hali ya juu, ulijua Kuna siku utatoboa, na sisi kama Serikali tupo nyuma yako kuhakikisha kwamba hii Huduma uliyoianzisha inafika mbali zaidi, ametoa Ajira amekomboa familia nyingi”
Amesisitiza kuwa ili Nchi iweze kuendelea ni lazima kuwepo na Sekta binafsi hivyo ni muhimu Kwa wao kutumia fursa zinazotengenezwa kupitia Serikali katika kuweka mazingira wezeshi ikiwemo uboreshaji wa miundombinu kama Reli ya Mwendokasi SGR ambapo itawezesha watu wengi kutengeneza vipato.
“Saivi SGR italeta watu wengi kila siku hapa Dodoma ambao wataingia na kutoka, Nidhamu, Ubunifu ndio Siri ya mafanikio” amesema
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Vio Juisi Bi. Vaileth Mwashiuya amesema kufanikiwa kwake kumetokana na kujituma ambapo alianza Kwa kutembeza mtaani na Sasa kufikia hatua ya kufungua Ofisi jambo ambalo haikuwa j rahisi na kupitia kwake atakwenda kuzalisha Ajira na kuwasaidia waliokata Tamaa ikiwemo kutoa Darasa la kuwafundisha utengenezaji na Biashara ya Juis ili waweze kujiajiri.
Pia malengo yake ni kufungua matawi katika mikoa mingine ili kupanua zaidi wigo wa fursa za Ajira katika maeneo mbalimbali.
Ametoa Wito kwa Watanzania kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo ili kutimiza malengo.