WIZARA YA MADINI, KAMPUNI YA PREDICTION SOFTWARE INC WAJADILI MFUMO BORA WA BIASHARA YA MADINI

0

Wizara ya Madini imekutana na Kampuni ya Prediction Software Incorporated kutoka Nchini Marekani na kujadili mfumo bora wa kuboresha biashara ya madini hapa nchini kwa njia ya kidijitali na teknolojia ya kisasa.

Kikao hicho kimefanyika leo Julai 24, 2024 katika Ofisi za Wizara ya Madini zilizopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, ambapo Rais wa Prediction Software Inc., Gene Chandler, amewasilisha mfumo wa kiteknolojia wa kufuatilia na kudhibiti biashara ya madini ya Metali yakiweno Dhahabu (The Mineral Trading Management System – Gold Tracker).

Katika wasilisho hilo, Gene Chandler ameeleza kuwa mfumo huo wa kidijitali unalenga kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Sekta ya Madini hususan katika ufuatiliaji, udhibiti, na utoaji sahihi wa hesabu.

“Mfumo huu unahusisha utoaji leseni, ukusanyaji wa mirabaha, tozo, na biashara ya Madini ya Metali kama Dhahabu. Kwa kutumia The Gold Tracker na XRF Precious Metal Analyzers, wateja wanaweza kuongeza mapato yao kupitia ukusanyaji sahihi na wa haraka wa ushuru na kodi, huku pia wakilinda mazingira na rasilimali za nchi kupitia usimamizi bora wa leseni” amesema Chandler.

Chandler ameendelea kueleza kuwa teknolojia hii tayari imeshatumika katika nchi kadhaa, ikiwemo Marekani, Canada, Australia, na Afrika ya Kusini imeonyesha mafanikio makubwa katika kuboresha usimamizi na biashara ya madini. Amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuzingatia matumizi ya teknolojia hii ili kufikia viwango vya kimataifa katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, amesema kuwa hivi sasa biashara ya dhahabu nchini Tanzania inatumia mfumo ambao katika usimamizi wake una baadhi ya changamoto katika ufuatiliaji wa biashara ya madini hayo.

Dkt. Mwanga amesema kuwa wataalam wa Wizara watakaa na kujadili kwa kina kuhusu mfumo huo wa teknolojia ya kisasa uliowasilishwa na Prediction Software Inc., na kwamba lengo ni kuona jinsi mfumo huo unavyoweza kutumika kwa ufanisi nchini Tanzania ili kuboresha usimamizi wa madini na kuongeza mapato ya Serikali.

“Teknolojia inaweza kusaidia katika kufuatilia shughuli za uchimbaji madini, kudhibiti biashara haramu ya madini, na kuhakikisha kuwa ushuru wote unakusanywa kwa usahihi na kwa wakati” ameongeza Dkt. Mwanga.

Wajumbe wa kikao hicho wamejadili kwa kina manufaa ya mfumo wa The Gold Tracker & XRF Precious Metal Analyzers na jinsi unavyoweza kusaidia kuboresha sekta ya madini nchini. Pia wamejadili kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mfumo huo na jinsi ya kuzitatua.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano kwamba wataalam wa Wizara ya Madini wataendelea kufanya tathmini kwa ajili ya hatua zaidi. Hatua hiyo ni muhimu katika juhudi za Serikali kuboresha usimamizi na biashara ya madini nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *