WAFUGAJI WALIOPIMIWA MASHAMBA WAPEWE FURSA ZA UFUGAJI WA KISASA – RC SENYEMULE

0

Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, wameagizwa kuwasiliana na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuwatafutia fursa wafugaji walioitikia wito wa kupima maeneo yao kwa hiari na kufanikisha kupatiwa hati miliki za ardhi na mashamba.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule alipohudhuria hafla fupi ya kukabidhi hati miliki za mashamba ya wafugaji wa Kijiji cha Fufu ndani ya Wilaya ya Chamwino Julai 23, 2024.

“Wafugaji wamekubali kufuga ndani ya maaeneo yao. Serikali lazima tuwaunge mkono ili waone matunda ya dhamira yao. Wakurugenzi, muwasiliane na Wizara ya Kilimo ili wafugaji hawa wapate fursa ya kuchimbiwa visima, wafundishwe upandaji wa majani ya chakula na wapate mbegu za kisasa za mifugo” Amesema Mhe. Senyamule.

Akitoa taarifa ya upimaji mpaka kutolewa kwa hati hizo, Afisa MaendeleoArdhi Wilaya ya Chamwino Bw. Enock Mligo amesema maeneo yaliyopimwa ni katika tarafa za Makang’wa na Itiso amabzo zina wafugaji wengi na ndizo zimekithiri kwa migogoro ya ardhi kati wakulima na wafugaji hivyo zoezi hilo limepunguza kwa kiasi kukubwa migogoro hiyo.

Jumla ya hati 11 kati ya 20 zimekabidhiwa ambapo zoezi la upimaji lilitambua wakulima 87 na mashamba 1317 pamoja na ekari 6639.16 zimepimwa. Licha ya upimaji huo, wafugaji hao wametakiwa kufuata masharti ya umiliki ardhi ikiwa ni pamoja na kutunza alama za mipaka na kutunza mazingira.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa alitumia Mkutano huo kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Fufu na vijiji jirani waliojitokeza ambapo miongoni mwa kero zilizowasilishwa ni pamoja na changamoto ya maji, umeme, upungufu wa walimu, eneo la mnada, barabara, kituo cha afya, n.k

Wataalamu walioambatana na Mkuu wa Mkoa walitoa majawabu kwa kero hizo wakisema miradi ya maji na umeme ipo kwenye utekelezaji na pindi itakapokamilika, itamaliza kero hizo. Maeneo kwa ajili ya kituo cha afya na mnada yapo tayari bado utekelezaji wake. Mhe. Senyamule alitoa muda wa juma moja kupata taarifa juu ya utekelezaji wa utatuzi wa kero zote zilizowasilishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *