WAJASIRIAMALI SHIRIKIANENI NA KUBUNI MBINU-MBUNGE TAUHIDA
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi Mhe.Tauhida Gallos amewataka wajasiriamali kushirikiana na kubuni mbinu mbalimbali zitakayoweza kuwaletea maendeleo katika familia zao.
Mhe. Tauhida ameyasema hayo huko Mazizini mara baada ya kukabidhi Majiko ya Gesi na Sare kwa Wajasiriamali wa Diko la Mazizini Wilaya ya Magharibi B.
Amesema Serikali zote mbili zimeweka mikakati ya kuwawezesha Wanawake kiuchumi hivyo ni vyema kujiunga pamoja ili kufikia malengo hayo ya kujikwamua na tatizo la umasikini.
Aidha amewataka kujali na kuthamini kazi yao kwani imekuwa ikiwasaidia kwa kiasi kikubwa kupata mahitaji muhimu ikiwemo kusomesha Watoto wao.
Hata hivyo ameahidi kuzifikisha sehemu husika changamoto zinazowakabili wajasiriamali hao ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wake Mkuu wa Diko wa Diko la Mazizini Hashim Omar Haji amesema umoja huo umeweza ukiwaunganisha Wanawake hao Kisasa, Kiuchumi na kimaendeleo.
Hivyo amewataka kuendelea kushirikiana ili kuzidi kukuza umoja na mshikamano walionao.
Nao Wajasiriamali wa Diko la Mazizini wameomba kupatiwa ufumbuzi matatizo yanayowakabili ikiwemo vitendea kazi, Wafadhili na mafunzo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo wamesema hali itawawezesha kufikia malengo waliojipangia ya kujikwamua na tatizo la umasikini na kuepukana na hali tegemezi.