UMEME KUONGEZA UZALISHAJI WA MADINI MKOA WA KATAVI-MAVUNDE
Waziri wa Madini Mh . Anthony Mavunde amewaeleza wachimbaji wa mkoa wa Katavi kwamba utekelezaji wa mradi wa kuingiza Katavi kwenye gridi ya Taifa itasaidia upataikanaji wa uhakika wa umeme na hivyo kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa madini mkoani Katavi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo jana Mpanda,Mkoani Katavi wakati wa kikao cha pamoja kati yake na uwakilishi wa wachimbaji mkoani Katavi ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kikazi ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muunganonww Tanzania Dkt. Samia S. Hassan mkoani humo.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa utekelezaji mkubwa wa mradi wa umeme ambao umelenga kuuingiza mkoa wa Katavi kwenye gridi ya Taifa na hivyo kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Nategemea baada ya Katavi kuingia kwenye gridi ya Taifa,uzalishaji wa madini utaongezeka maradufu kuliko hivi sasa na hivyo kupelekea kuongezeka kwa mapato yatokanayo na sekta ya madini.
Kuhusu suala la tozo zinazongezeka mara kwa mara kupitia Mamlaka za Halmashauri za Wilaya na Manispaa,tutakutana na Waziri wa TAMISEMI ili tulizungumze hili kwa pamoja na kulipatia muafaka jambo hili”Alisema Mavunde
Akitoa salamu za wachimbaji Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Katavi (KATAREMA) Ndg. William Mbogo ameishukuru serikali na Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa utashi wake wa kukuza sekta ya madini nchini kwa kuiongezea Bajeti Wizara ya Madini kufikia Tsh 231bn ili kusaidia kufanya utafiti wa kina nchi nzima na kuwatoa wachimbaji kwenye kuchimba kwa kubahatisha.
Aidha amemuomba Waziri wa Madini kushughulikia matatizo yaliyowasilishwa kwake kimaandishi ikiwemo suala la upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika na tozo zilizokithiri zilizotambulishwa na Halmashauri za Wilaya na Manispaa ambazo zinakwenda kuathiri suala la uchimbaji wa kiasi kikubwa.