DK.MWINYI: MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI YAMEIMARISHA SEKTA YA SUKARI

0

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yameleta mafanikio makubwa na kuwezesha kuongezeka kwa uwekezaji mkubwa wa mitaji katika sekta ya sukari.

Aidha, ametoa rai kwa nchi Wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia fursa walizonazo kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji ili kukuza uwekezaji katika uzalishaji wa sukari.

Akifungua leo Julai 10, 2024 Mkutano wa wazalishaji wa sukari wa nchi za SADC uliofanyika Zanzibar, Dk.Mwinyi amesema mazingira hayo mazuri yamechagiza viwanda vyote hapa nchini kufanya upanuzi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari

“Sekta ya sukari ni sekta iliyopewa kipaumbele katika kilimo cha nchi kwa kuwa viwanda vya sukari ni vitovu muhimu vya kilimo na uchumi Tanzania na pamoja na umuhimu huu, uzalishaji wa sukari kwenye nchi yetu ni moja ya nyenzo kuu na muhimu ya kuimarisha na kulinda usalama wa chakula, kwa kuwa sukari ni moja ya chakula muhimu nchini,”amesema.

Aidha, amesema uzalishaji wasSukari ndani ya Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine wanachama wa SADC zinazozalisha Sukari, huokoa matumizi ya fedha nyingi za kigeni kila mwaka ambazo zingetumika kuagizia Sukari nje ya nchi, kama Sukari isingezalishwa kwenye nchi.

“Ni dhahiri kuwa, kujenga mazingira bora na kuondoa vikwazo vya uwekezaji katika Sekta ya Sukari kwenye nchi zetu kutawezesha kustawisha zaidi masoko ya ndani ya nchi za SADC na kuongeza fursa ya biashara ya Sukari katika Soko la pamoja la Afrika (AfCFTA) na Dunia kwa ujumla,” amesema.

Amepongeza nchi wanachama wa SADC kupitia utaratibu rasmi wa kuendeleza sekta ya sukari kupitia biashara ya SADC na kusema kuwa serikali itaendelea kuweka na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili sekta ya sukari barani Afrika iweze kuwa na ushindani na kuleta manufaa zaidi kwa wananchi.

Pamoja na hayo, Dk.Mwinyi, alisema imani yake mkutano huu utatoa fursa kwa wadau wa sekta ya sukari kubadilishana mawazo na uzoefu kwa lengo la kuimarisha mazingira wezeshi kwa maendeleo endelevu ya Sekta ya Sukari katika nchi wanachama wa SADC na Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *