SHEKHATI ZEANA – MIKOPO YA KAUSHA DAMU CHAZO MMOMONYOKO WA MAADILI
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Mkoa wa Singida, Shekhati Zeana Saidi, amesema madeni ya kwenye vikoba na mikopo ya kausha damu imekuwa chanzo cha mmonyoko wa maadili hapa nchini.
Zeana amesema hayo jana wakati akihutubia wanawake wa JUWAKITA Wilaya ya Iramba mkoni Singida kwenye Maulidi ya kumswalia Mtume Mohammad ( S.A.W) yaliyofanyika Masjid Ajib wilayani hapa.
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na harambee ya upatikanaji wa fedha za umaliziaji wa ujenzi wa madarasa ya kinamama.
Shekhati Zeana amesema imefika wakati kwa kinamama kupunguza mikopo ili waweze kupata muda wa kukaa na famili zao na kulea watoto, kuliko kutumia muda mwingi kwenye magenge ya nyaya na biashara zingine.
“Sisi kinamama tumeacha majukumu yetu ya msingi nakwenda kufanya kazi za kinababa maana saivi kinamama ndio tunalisha familia ,kinababa wenyewe wako bize na vijiwe vya kahawa tu, nani sasa atatazama watoto au kusikiliza kero zao kama sisi wazazi tupo bize na kutafuta pesa,” alisema Zeana.
Alisema kama wanawake ndio wanachukua jukumu la kulisha familia je watapata wapi muda wa kuangalia watoto kweli zaidi ya kuwaza madeni ya vikoba na mikopo ya kausha damu.
“Ifike wakati akina mama tubadilike kila mtu afanye majukumu yake baba alishe familia yake na mama aangalie watoto wake hapo ndio tutakuwa tumepona na kupunguza mmomonyoko wa maadili katika familia zetu na jamii yetu kwa ujumla,” alisema Zeana.
Naye Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Al-Haaj Buruan Mlau alipongeza na kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye elimu hivyo tuwatoe watoto wetu wenye ulemavu na wasio walemavu wakasome.
Alisema wazazi lazima watambue kuwa watoto wakiwa na elimu hata vitendo viovu vitapungua kwa kasi sana kwenye jamii na pia tupende kusoma elimu ya dini pamoja na ya dunia zitatusaidia sana katika maisha yetu na kupunguza ukatili kwa watoto.
Mlau aliwataka waumini wa sini ya kiislamu na wananchi waliofika kwenye Maulidi hiyo kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kwenye uchanguzi wa serikali za mitaa unaitarajia kufanyika mwaka huu.
“Kama tutajitokeza kwa wingi kuchagua vingozi basi twende tukachague viongozi bora na sio bora viongozi wasio na hofu ya Mungu watatupoteza tukachague viongozi wenye hofu ya Mungu na wenye maadili na huruma na wananchi,” alisema Mlau.