WIZARA YA FEDHA YAPONGEZWA KWA KUANDAA YALIYOMO KWENYE BAJETI YA SERIKALI KWA LUGHA NYEPESI

0

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles Kichere, ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa yaliyomo kwenye Bajeti ya Serikali kwa lugha nyepesi (Toleo la Mwananchi) kwa kuwa inamsaidia mwananchi kuielewa bajeti ya nchi.

Bw. Kichere ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha wakati wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa kijitabu hicho ni sehemu ya uwazi na uwajibikaji kwa kuwa mwananchi wa kawaida anaweza kuelewa mipango ya Serikali katika kutekeleza maendeleo yao.

Aidha, alisema kuwa watoa huduma katika banda hilo wanaonesha umahiri katika kuelezea masuala mbalimbali, jambo ambalo litasaidia kuongeza uelewa kwa umma kuhusu Sera na Majukumu ya Wizara.

Kwa upande wake Mchumi Mkuu wa Idara ya Usimamaizi wa Bajeti, Bw. Boniface Kilindimo, alisema kuwa Bajeti ya Serikali Toleo la Mwananchi ni kijitabu kinachotafsiri mipango na bajeti ya Serikali kwa muhtasari na lugha rahisi inayoweza kueleweka kwa mwananchi na wadau mbalimbali.

Alisema kuwa Kijitabu hicho kinasaidia kufahamu mipango na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka husika na jinsi bajeti inavyoweza kutatua changamoto na kuhamasisha dhana ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *