AWESO AIPANGUA DAWASA, AIWEKA CHINI YA UANGALIZI MAALUM

0

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemtaka Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), Kiunga Kingu akae pembeni kwa muda, pia amemsimamisha kazi, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji-DAWASA, Shaban Mkwanywe na kuanzia leo June 30,2024 ameiweka DAWASA chini ya uangalizi Wizara ili kuboresha utendaji wake kufuatia uzembe uliopelekea visima kukosa maji na kufanya Wakazi wa Dar es salaam kukosa maji.

Aweso ametangaza uamuzi huo leo baada ya kufanya ziara ya kimkakati na ya kushtukiza katika Ofisi za DAWASA zilizopo Ubungo Dar es salaam ili kupata maelezo ya Watendaji ya sababu za Watu kukosa maji na baada ya kushindwa kuridhishwa na majibu aliamua kuzungukia matanki ya maji katika maeneo manne tofauti ikiwemo la Ardhi UDSM na Kibamba huku akituma Timu nyingine kwenda kukagua matanki ya Kigamboni ambapo matanki hayana maji huku mengine yakiwa na maji kidogo ukilinganisha na mahitaji ya Wananchi huku Watendaji wa DAWASA wakishindwa kueleza sababu iliyopelekea uhaba huo wa maji.

Aweso amesema “Mwanzoni kulipokuwa kunakosekana maji tulikuwa tunasema shida ni vyanzo vya maji vimekauka hakuna maji, TANESCO umeme hamna lakini leo vyanzo vyote vina maji, umeme upo, niambieni kwanini hatuna maji kwenye matenki?, kwanini Wananchi wanateseka, wanalalamika wanapiga kelele kwenye Serikali?”

Ziara ya Aweso leo imekuja baada ya ziara ya Katibu Mkuu wa Maji aliyoifanya kwa siku mbili kujionea utendaji kazi wa DAWASA na hali ya upatikanaji wa maji ambapo amebaini uzembe aliouwasilisha kwa Waziri Aweso leo ikiwemo miundombinu ya maji kuwa chakavu, maji kupotea bila usimamizi, Watendaji wa DAWASA wa ngazi za chini kutopewa stahiki zao muhimu na kupelekea kufanya kazi bila hamasa nzuri na hata kupelekea kuwajibu vibaya Wateja, ziara hiyo ya Aweso na Katibu Mkuu itaendelea katika maeneo mbalimbali ya Nchi ili kuboresha upatikanaji wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *