TANROADS YAGAWA VIFAA VYA KUPIMA UMBALI WA MKONGO WA MAWASILIANO
Mkurugenzi wa Matengenezo wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Dkt. Christina Kayoza, amegawa vifaa vya kupima umbali wa Mkongo wa Mawasiliano (OTDR) inayotumika na makampuni ya simu ndani ya hifadhi ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS .
Zoezi hilo limefanyika leo jijini Dar es Salaam Juni 28, 2024 kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta, kwenye kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa matengenezo ya barabara kwa Mikoa ya kanda ya Pwani na Morogoro kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Vifaa hivyo vimetolewa kwa Mameneja wa TANROADS ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga na Pwani ili kuweza kuwasaidia katika upimaji wa umbali kwenye Mkongo wa Mawasiliano kwenye hifadhi ya barabara.
Uwepo wa vifaa hivyo, utaongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa watumiaji wa Hifadhi ya Barabara hususani Mikongo ya simu.
Mbali na ugawaji huo, pia Mha. Dkt Kayoza , amesisitiza utunzaji wa Vifaa hivyo na kuanza utekelezaji wa kuvitumia.