MKATABA UJENZI WA JENGO LA GHOROFA 8 LA TGC WASAINIWA
Wizara ya Madini imesaini Mkataba wa Ujenzi wa Jengo la kisasa la ghorofa nane la Kituo cha Jemolijia Tanzania (TGC) na Kampuni mbili za wazawa zilizoungana za Skywards na Lumocons.
Hafla hiyo imefanyika leo Juni 26, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Prof. AbdulKarim Mruma jijini Dodoma na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa.
Kwa upande wa Wizara, Mkataba ho umesainiwa na Katibu Mkuu Kheri Mahimbali huku Mkurugenzi wa Kampuni Lumocons Limited Innocent Shirima akisaini kwa niaba ya Kampuni hizo mbili za ujenzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kiruswa amewataka wazabuni hao kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa ubora na muda unaotakiwa na kwamba Wizara ya Madini itatoa ushirikiano ili kuhakikisha kutokuwepo kwa vikwazo vyovyote muda wote wa ujenzi.
“Niwapongeze kwa kushinda zabuni hii, lakini niwaeleze kuwa ujenzi wa mradi huu utawafikisha mbali na kuwatangaza kama mtatimiza yote yaliyopo kwenye mkataba huu” amesema Dkt. Kiruswa
Aidha, ameelezea umuhimu wa jengo hilo kwa kusema kuwa miundombinu iliyopo sasa haikidhi mahitaji ya Kituo hicho ambacho pia kina chuo cha kuongezea thamani madini ya vito, hivyo kukamilika kwa mradi huo utasadia sana katika utekelezaji wa shughuli za kituo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kuwa lengo la Wizara ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini ya vito barani Afrika na kwamba Serikali iko mbioni kurejesha Minada ya Madini ya Vito na bidhaa za vito, hivyo kukamilika kwa mradi huo utasadia katika Uongezaji Thamani Madini hayo hapa nchini kwa wingi na kwa ubora vya kimataifa.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lumocons ameishukuru Wizara ya Madini kwa kuwaamini na kutoa zabuni hiyo na kusema kuwa watatekeleza ujenzi wa mradi huo kwa ubora, kiwango na wakati kwa mujibu wa mkataba, huku akisema ni fursa kubwa kwao kama Kampuni za wazawa.
Ujenzi wa Jengo hilo la TGC utagharimu kasi cha shilingi bilioni 33.42 (33,429,365,267.00) mpaka kukamilika.
TGC ni kituo kinachojihusisha na kutoa elimu, mafunzo, na huduma mbalimbali zinazohusiana na madini na vito vya thamani. Majukumu yake ni pamoja na kutoa mafunzo ya uongezaji thamani madini ya vito ikiwemo kukata, kung’arisha na huduma za kitaalam kwa wafanyabiashara na watengenezaji wa vito kuhusu uongezaji thamani madini hayo.