KLINIKI YA USHAURI NA ELIMU YA SHERIA KWA UMMA YAZINDULIWA

0

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amezindua Kliniki ya Ushauri na elimu ya Sheria kwa Umma inayokusudia kusogeza huduma za msaada wa kisheria kw Wananchi ili kupunguza migogoro mbalimbali miongoni mwa jamii na kupata suluhu ya changamoto za kisheria zinazowakabili.

Kliniki hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili wa Serikali ni agizo la Rais wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka viongozi kuwa na utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya Wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaongoza katika taratibu za kupata haki. 

Akizindua Kliniki hiyo leo tarehe 26 Juni 2024 Jijini Dodoma, Dkt. Feleshi amesema Kliniki hiyo itaimarisha utawala wa Sheria Nchini ikiwemo kuchochea mazingira ya amani kwa wawekezaji ndani na nje ya Nchi. 

“Kipekee natoa rai kwa Mawakili wote wa Serikali hapa nchini kutenga muda na kusikiliza wananchi kupitia maeneo yao, niwakumbushe pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao bado hawajakamilisha kuteua wajumbe wawili wa kamati za ushauri wafanye hivyo ili kamati hizo zianze kusikiliza malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, “amesema

Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali amevikumbusha vyama vya Mawakili wa Serikali (TPBA)pamoja na Mawakili wa Tanganyika (TLS)kuendelea kushirikiana na Serikali na kamati za ushauri wa kisheria ngazi za Mikoa na Wilaya ili kusikiliza malalamiko ya Wananchi na kuyatatua kwa wakati. 

Amesema Kliniki zitakazo endeshwa na Kamati hizo zitakuwa endelevu kwa nchi nzima na hivyo kuwataka Wananchi wa Dodoma na Mikoa jirani kujitokeza kupata huduma ya Ushauri wa kisheria bure kuanzia June 26 hadi Julai 3,2024 kuanzia saa 2.00 asuhubi hadi saa 10.00 jioni.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo ameeleza kuwa wananchi wakiendelea kutatuliwa kero zao uzalishaji utakua kwa kasi. 

Amesema Serikali kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Wananchi wamekuwa sehemu ya mabadiliko kwa kuelewa namna ya kutafuta suluhu ya malalamiko yao. 

“Kezo za wananchi ni wajibu wetu, tuendelee kuwa pamoja katika kuzitatua kupitia ushirikiano wetu, kupitia hizi siku zilizoyengwa Wananchi wataendelea kuzitumia vizuri kuelimishwa zaidi ili wapate haki yao na kuwa na amani, ” amesema

Amesisitiza kuwa wataendelea kuboresha mifumo ya msaada wa kisheria kupitia simu janja na simu za kawaida ili kufanikisha huduma bora kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *