MPINA AFUNGIWA VIKAO 15 VYA BUNGE

0

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amefungiwa kuhudhuria vikao 14 vya Bunge kuanzia leo Juni 24, 2024 baada ya ‘kutiwa hatiani’ kwa kosa kukiuka kanuni za Bunge, kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge.

Mpina amepewa adhabu hiyo baada ya wabunge kuchangia hoja ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo baada ya uchunguzi wake ilipendekeza mbunge huyo apewe adhabu ya kutohudhuria vikao visivyopungua 10.

Mpina ametiwa hatiani baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwa spika kabla ushahidi huo haujawasilishwa mezani au kupewa idhini na bunge kufanya hivyo.

Mbunge huyo aliwasilisha ushahidi baada ya kusema bungeni kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alilidanganya Bunge kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo kiwango cha upungufu wa sukari nchini, kwamba kampuni zilizopewa vibali vya kuagiza sukari hazikuingiza sukari nchini na kwamba waziri alikataa kufanya kikao na wadau wa sukari.

Kufuatia adhabu hiyo, Mpina hatohudhuria vikao vya Bunge la Bajeti vilivyosalia, hatohudhuria Bunge la Septemba na ataanza kushiriki kikao cha pili cha Bunge la Novemba mwaka huu.

Baada ya kupewa adhabu hiyo, spika alimtaka Mpina ambaye alikuwa ndani ya ukumbi wa Bunge kutoka ndani ya ukumbi, ikiwa ni mwanzo wa kutumikia adhabu yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *