WIZARA YA FEDHA YASHAURIWA KUWAFIKIA WANANCHI WOTE

0

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, ameishauri Wizara ya Fedha kuhakikisha Watanzania wote nchini wanapatiwa elimu ya fedha ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha na waweze kufanya maamuzi sahihi katika matumizi sahihi ya vipato vyao.

Bi. Quintine ametoa ushauri huo alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani Urambo mkoani Tabora, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Fedha na kujikomboa kiuchumi.

“Naamini Wananchi wote wakipatiwa elimu hii muhimu ya masuala ya fedha wataweza kuwa na nidhamu ya matumizi lakini pia watakuwa na uelewa wa wapi wakawekeze fedha zao ili kuongeza mitaji katika biashara zao na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”, alisema Bi. Quintine.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bw. Sabhi Makongo, alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali ya masuala ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ikiwemo watumishi, wanavikundi vya kinamama na Jamii katika ngazi ya familia.

“Elimu ya fedha inahitajika sana kwa wananchi wa makundi mbalimbali hivyo sisi kama Halmashauri tutaendelea kutoa elimu hii mara kwa mara kwa wananchi wetu na kuwahamasisha kusajili vikundi vyao ili viweze kutambulika rasmi endapo fursa za mikopo zitatokea waweze kupata na kuongeza mitaji yao” alisema Bw. Makongo.

Naye mkazi wa Wilaya ya Urambo Bi. Chiku Rajabu, alisema kupitia mafunzo aliyoyapata yamempa uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia uwekezaji.

“Naishukuru sana Serikali kuona umuhimu wa elimu hii kutufikia sisi wana Urambo, hakika elimu niliyoipata itanisaidia kupanga mipango sahihi katika matumizi ya fedha zangu”, alisema Bi. Rajabu.

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema wapo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha.

“Katika utoaji elimu tunaonesha filamu ambayo imebeba mada mbalimbali ikiwemo masuala ya kujiwekea akiba, mikopo, kujiandaa na kustaafu, uwekezaji na bima”, alisema Bi. Bulugu.

Katika zoezi la kutoa elimu kwa Wananchi Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha imeambatana na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ikiwa ni Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *