WANANCHI WA TABORA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MASOKO YA MITAJIRAS TABORA

0

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya amewataka Viongozi, Watumishi na Wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Masoko ya Mitaji kwenye Taasisi rasmi zilizopewa dhamana na Serikali kufanya shughuli za uwekezaji kisheria ili kuweza kupata faida na kujikwamua kiuchumi.

Dkt.Mboya, alitoa rai hiyo alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wamefika mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.

“Wananchi mkoani Tabora tuamke, tutumie vizuri elimu ya fedha tuliyoipata hususan katika eneo la Uwekezaji ili tuweze kufanya maamuzi sahihi katika kuwekeza ikiwemo kupelekeza fedha sehemu sahihi ili uweze kupata faida”, alisema Dkt. Mboya.

Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha katika mikoa mbalimbali na kuwahamasisha wananchi kutumia taasisi rasmi za fedha zinazotambuliwa na Serikali.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Uyui, Bw. Cledus Mbawala, alisema kuwa katika ngazi ya Wilaya, Ofisi yake imekuwa ikifanya ufuatiliaji na kuhakikisha Taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya fedha zinakuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania na zinafuata sheria na taratibu katika kutekeleza majukumu yake.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema kuwa wamefika mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya nne za Uyui, Urambo, Sikonge na Tabora Manispaa.

“Tunawapongeza wananchi kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha kwa kuwa itawasaidia kupanga matumizi ya fedha wanazopata, wataweza kujiwekea akiba, watakuwa makini kuchukua mikopo kwenye Taasisi rasmi, za fedha na watafanya uwekezaji na kujikwamua kiuchumi”, alisema Bi. Bulugu.

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha katika mikoa ya Tabora, Simiyu na Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu ili kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *