TANZANIA KUOKOA MABILIONI UJENZI WA TANZANIA TWIN TOWER KENYA

0

Serikali ya Tanzania Juni 18, 2024 imezindua rasmi ujenzi wa majengo pacha jijini Nairobi, Kenya yatakayotumika na ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo na kitega uchumi.

Ujenzi huo utakaogharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF utajengwa katika eneo la kibiashara katikati ya jiji la Nairobi kwenye eneo ambalo Serikali ya Kenya iliipa Tanzania kwa ajili ya kujenga ofisi zake za ubalozi.

Akizungumza katika tukio la uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpya wa serikali kuhakikisha inatumia maeneo na majengo yake yaliyopo ughaibuni kuingiza fedha za kigeni badala ya kutumia fedha za serikali kuendesha ofisi hizo.

Waziri Makamba amesema mkakati wa serikali unataka kuiondoa Tanzania kutoka kutumia kiasi cha shilingi bilioni 29 kwa mwaka kulipa kodi kwenye balozi zake ughaibuni na badala yake kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 36 kwa mwaka kama mapato ya uwekezaji kama huo wa unaofanyika Kenya.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Walemavu), Deo Ndejembi, amesema mradi huo umefanyika baada ya upembuzi yakinifu wa kina uliofanywa na kubainisha faida itakayopatikana baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *