“NHC TUTAENDELEA KUJENGA NYUMBA ZENYE GHARAMA NAFUU”

0

Shirika la Nyumba la Taifa NHC limesema litaendelea kujenga nyumba zenye gharama nafuu ili wananchi waweze kumiliki nyumba kwa urahisi kupitia Miradi mbalimbali ya Shirika.

Kauli hiyo imetolewa leo 19 Juni, 2024 na Afisa Mkuu, Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Ndg. Emmanuel Lyimo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea Jijini Dodoma katika Viwanja vya Chinangali Park.

Maadhimisho hayo yamefunguliwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene

Afisa Lyimo ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajitokeza katika viwanja hivyo ili kupata uelewa na urahisi wa namna gani anaweza kumiliki Nyumba, ambapo kwa sasa Shirika hilo linajiandaa na utekelezaji wa mradi Mkubwa wa Medeli Jijini Dodoma huku likijivunia miradi yake mbalimbali ikiwemo Samia Housing Scheme, Morocco Square, Nyumba Elfu Moja Iyumbu ambao mpaka sasa Nyumba ambazo hazijanunuliwa zimesalia 78 Pekee.

“Tumekuja kuwaeleza watanzania wote kuhusu miradi tuliyonayo ambayo ni ya Nyumba za Makazi, Ofisi, Hoteli, Maduka nakadhalika, vilevile tuna mradi mpya ambao upo Medeli ambapo tutajenga nyumba Mia moja za Kisasa ambazo zitakuwa na huduma zote muhimu ikiwemo lifti, maegesho ya magari, Ulinzi, hivyo tunatoa wito kwa watanzania wote wafike katika Ofisi zetu Mkoa wa Dodoma kwaajili ya kuweza kupata nyumba” Amesema Afisa Lyimo

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano anaoendelea kulipatia Shirika hilo.

Akihutubia wakati wa Kufungua Maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewatahadharisha Watumishi wote wa Umma Watumishi ambao hawendani na kasi ya utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita na kusema Hawatawavumilia watumishi wasio na maadili, wazembe, au wale wasiomjali mwananchi na kutaja baadhi ya changamoto zilizopo kwenye Baadhi ya Sekta ikiwemo Ardhi ambapo ameeleza kushangazwa na Utatuzi wa Migogoro kufanyika katika kila ngazi kwani hupelekea Viongozi wasio waadilifu kujinufaisha kupitia Migogoro ya Ardhi

“Pale ambapo tutabaini utovu wowote wa nidhamu hatutasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu.kinachokosekana katika sekta ile ni ukiukaji wa Sheria, ambapo kuna udanganyifu mwingi na baadhi ya watumishi wa sekta kutokutimiza wajibu wao, na upungufu wa watumishi”Amesema Simbachawene

Katika eneo hilo Mhe. Simbachawene amekiri kuwa hata yeye ameshawahi kuingiliwa katika Ardhi ambayo ilikuwa ni haki yake aliyoimiliki kwa hati zake halali.

Maadhimisho hayo yanafanyika Jijini Dodoma kuanzia 16 Juni-23, 2024

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *