MAWAZIRI PROF. KITILA NA BASHE WASHUHUDIA UTIAJI SAINI MIKATABA MITATU UWEKEZAJI MKULAZI

0

Imeelezwa kuwa viwanda vingi hapa nchini vimekuwa vikijiendesha kwa kutumia malighafi zitokanazo na bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu hiyo ni kutokana urahisi wa upatikanaji wa malighafi hizo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameeleza hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba mitatu (3) iliyohusisha TIC (Kituo cha Uwekezaji Tanzania) na makampuni matatu tofauti, ikihusisha makabidhiano ya utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la kilimo Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro

Katika hafla hiyo iliyofanyika leo, Ijumaa Juni 14.2024 Dodoma City Hotel Prof. Kitila amesema sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa Tanzania kwa kuwa kilimo ndio sekta inayobeba pato la Taifa

“sekta ya kilimo imekuwa chanzo cha usalama kwa nchi kwa kuwa Tanzania inajitegemea kwa chakula kwa asilimia zote, na kwamba kutokana na hilo ndio maana sekta hiyo imekuwa ikiongoza kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi”

Katika hafla hiyo TIC kupitia Mkurugenzi mtendaji wake Gilead Teri amesaini mikataba hiyo sambamba na wawakilishi wa makampuni matatu (3) ya TFP (The Food Platform), Longping Agriscience na Eagle Hills

Akizungumzia mikataba hiyo Waziri Prof. Kitila Mkumbo ametoa wito kwa wawekezaji wote waliokabidhiwa eneo hilo kuhakikisha wanatekeleza makubaliano ya mikataba yao kwa wakati kama ambavyo matarajio ya serikali yalivyo, na kwamba serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu ili uwekezaji huo uoneshe tija kwa jamii.

Wakati huo huo, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewataka wawekezaji waliopewa kuwekeza kwenye eneo la Mkulazi, mkoani Morogoro kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira na vibarua kwa wakazi wanaozunguka eneo la uwekezaji Mkulazi kwa kuwa kufanya hivyo kutajenga msingi wa ushirikiano kwa jamii inayozunguka mradi huo

Amesema uzoefu unaonesha kuwa wawekezaji wanaotekeleza shughuli zao bila kuonesha ushirikiano na jamii inayozunguka eneo la uwekezaji wamekuwa wakipata wakati mgumu hasa linapokuja suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo

“serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mara zote imekuwa mstari wa mbele katika kuwalinda wawekezaji, hata hivyo inataka kuona wawekezaji wanatengeneza mazingira rafiki yatakayosaidia jamii wanayowekeza inanufaika kiuchumi kutokana na uwekezaji wao”

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema mradi wa utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la Kilimo Mkulazi, uliopo Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro utafungua fursa lukuki kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa namna moja au nyingine kwa kuwa viwanda vitakavyowekwa eneo hilo vitajikita kwenye sekta hizo za kiuchumi

Dkt. Kida amesema mashamba hayo yamekodishwa kwa wawekezaji na TIC ikiwa ni sehemu ya kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya biashara na uwekezaji, ambapo licha ya wakulima, wafugaji na wavuvi kunufaika na uwekezaji huo lakini pia wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na zisizokuwa za serikali watapata fursa ya kujifunza kuhusu kilimo na ufugaji wa kisasa kwenye eneo hilo

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Binilith Mahenge amesema uwekezaji huo unakuja ikiwa ni sehemu ya matokeo ya uvutiaji wawekezaji na kuwekwa kwa mazingira rafiki kwao kutoka kwa serikali ya awamu ya sita (6) inayoongoza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Amesema TIC imekuwa ikifanikisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kutoka sekta ya kilimo, hivyo baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo hatua inayofuata ni kwa TIC kuhakikisha uwekezaji uliokusudiwa unafikiwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *