SHERIA MPYA YA UNUNUZI WA UMMA KUANZA KUTUMIKA JUNI 17, 2024

0

WAZIRI wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitangaza tarehe 17 Juni, 2024 kuwa tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 455 la tarehe 7 Juni, 2024 lililochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 13 Vol. 105 la tarehe 7 Juni, 2024, uteuzi wa tarehe hiyo umezingatia kifungu cha 1 cha sheria hiyo.

Septemba 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha muswada wa sheria hiyo ya ununuzi wa umma, hatua iliyotoa nafasi kwa Serikali kukamilisha taratibu za kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, na kisha Waziri mwenye dhamana kutangaza kwenye gazeti la Serikali.

Akizungumzia baadhi ya mabadiliko yaliyowekwa kwenye sheria hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi, alisema kuwa sheria hii imetoa nafasi zaidi ya upendeleo kwa wazabuni wa ndani ya nchi pamoja na bidhaa zinazozalishwa au kuchimbwa ndani ya nchi.

Aliyasema hayo katika wasilisho lake wakati Mamlaka hiyo ilipotoa mafunzo kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, hivi karibuni jijini Dodoma.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alisema kuwa sheria mpya imepunguza muda wa michakato ya ununuzi wa umma, kuboresha masharti ya matumizi ya njia ya ‘Force Account’ kuwa kwa ajili ya miradi isiyozidi Shilingi Milioni 100, kuipa PPRA mamlaka ya kuweka ukomo wa bei, na kuweka sharti la lazima la kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) kwa kila mchakato wa ununuzi.

“Mfumo wa NeST utasaidia katika kuhakikisha tunaongeza ufanisi na uzingatiaji wa sheria ili kupata thamani halisi ya fedha. Nawasihi waheshimiwa wabunge, tukawahamasishe Watanzania kutumia Mfumo wa NeST na kukataa visingizio vinavyotolewa na baadhi ya watu wanaotaka kukwepa kuutumia kwa maslahi binafsi,” alisema Bw. Maswi.

Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kutoa mafunzo ya Mfumo wa NeST kwa wazabuni na taasisi nunuzi, na baada ya Julai 1, 2024 wataandaa mafunzo ya sheria mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *