WAZIRI MKUU ASISITIZA UDHIBITI WA FEDHA NA MALI ZA UMMA

0

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi watendaji wa Miji na Majiji kusimamia kikamilifu makusanyo na matumizi ya fedha zinazokusanywa na kupelekwa kwenye maeneo yao kwaajili ya maendeleo.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Juni 12, 2024 kwenye Mkutano mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya serikali za Mitaa, Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Arusha kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha AICC.

Mhe. Kassim Majaliwa amewataka watendaji hao kuwa na udhibiti wa mapato ya Halmashauri zao akikemea Wizi, ubadhirifu wa mali za umma na kuwataka washiriki wa mkutano huo kubuni mkakati wa udhibiti wa fedha za umma kwenye Halmashauri za Tanzania bara.

Waziri Mkuu pia ameonesha kusikitishwa na taarifa za baadhi ya Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri kutokufahamu kuhusu fedha zinazoingia na kutoka kwenye vituo vyao vya kazi, akisema jukumu hilo linalopaswa kusimamiwa kikamilifu na wakurugenzi hao.

Waziri Mkuu pia amewaagiza Wakurugenzi hao wa Halmashauri kufanya tathimini ya kimaendeleo kwenye maeneo yao na kutoa suluhisho la changamoto wanazozipitia katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi kama ilivyo dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu katika hatua nyingine amehimiza suala la nidhamu, uadilifu na uaminifu kwa watumishi wa Umma kote nchini Tanzania akikemea tabia za baadhi ya watumishi wa Umma ambao wamekuwa wakichafua taswira ya serikali katika ualidilifu wake kwenye kuwatumikia wananchi.

Mkutano wa TOA unafanyika kwa siku tatu Mjini Arusha ukiwahusisha Makatibu tawala wa Mikoa ya Tanzania bara, Wakurugenzi watendaji wa Majiji, Miji na Halmashauri zote 184 pamoja na maafisa wote wa Sekretarieti za mikoa na Halmashauri zote pamoja na Wakurugenzi wa manispaa zote na wasimamizi wa mamlaka za serikali za mitaa visiwani Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *