SERA YA UGATUAJI MADARAKA YATATIZA WANANCHI KUJIAMULIA MAMBO YAO
Mwenyekiti wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania TOA, Bw. Albert Msovella amesema kutokukamilika kwa Sera ya Ugatuaji wa madaraka ni kikwazo katika maboresho ya serikali za mitaa na uharaka katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Bw. Msovella ametoa kauli hiyo mbele ya Waziri Mkuu wakati wa hotuba yake ya Kumkaribisha Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Maboresho ya serikali za mitaa Tanzania leo Juni 12, 2024 kwenye kituo cha kimataifa cha Mikutano AICC mjini Arusha.
Msovella kadhalika amemueleza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwa kutokukamilika kwa sera hiyo kumekwamisha kuwa na dira moja yenye kutoa mwelekeo wa pamoja katika kutekeleza ugatuaji wa madaraka kwa wananchi katika kujiamulia mambo yao.
Aidha Msovella ameeleza pia changamoto ya kusitishwa kwa ruzuku ya serikali za Mitaa suala ambalo limetatiza halmashauri nyingi za Tanzania bara kukosa watumishi na vitendea kazi muhimu katika kutimiza ugatuaji wa madaraka kwa wananchi.
Akizungumzia faida ya ugatuaji wa madaraka, Bw. Msovella amesema ushiriki wa wananchi katika kujiamua maendeleo yao umeongezeka huku pia demokrasia, uwazi na uwajibikaji ukiongezeka kwa kiasi kikubwa kulinganisha na hapo awali.
Katika hatua nyingine Bw. Msovella ambaye pia ni Katibu tawala wa Mkoa wa Katavi ameiomba serikali kuendelea kuwajengea uwezo TOA ili kuendelea kushauri na kuelekeza baadhi ya mambo kwa serikali kuu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.