WAKAZI WA KIGOMA WAASWA KUJIHADHARI NA MIKOPO KAUSHA DAMU

0

Na Chedaiwe Msuya, WF, Kigoma

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Kanal Anthony Mwakisu amewataka Wananchi kukopa kwenye taasisi za fedha zilizosajiliwa na Serikali na kutambulika kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwa mkopaji kwa kuwa taasisi hizo zinaendeshwa kwa mujibu wa Sheria.

Kanalı Mwakisu alitoa rai hiyo baada ya kukutana na wataalam wa Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Benki Kuu na wataalam wengine kutoka Taasisi za Serikali waliofika Wilayani mwake kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kwenda kukopa Fedha kwenye benki na Taasisi nyingine za fedha zilizosajiliwa na zinazotambulika kisheria na siyo kwenda kukopa Fedha kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa na serikali.

“Matumizi ya Fedha ni muhimu sana, hivyo wananchi wasikope tu kwenye vikundi ambavyo havijasajiliwa”. Amesisitiza Kanali Mwakisu.

Aidha, Kanali Mwakisu alisema kuwa Serikali imekusudia kuhakikisha wananchi wengi wanapata uelewa wa masuala ya fedha ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika huduma rasmi za fedha.

“wakulima msifanye matumizi mabaya ya Fedha zenu mnapo vuna mazao yenu bali fedha hizo zitumieni Kwenye matumizi sahihi ikiwemo kupeleka watoto shule”. Aliongeza Kanali Mwakisu

Kwa upande wake Bw. Stanley Kibakaya ambaye ni Afisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, aliwataka wananchi wanapokopa waangalie viwango vya riba ndipo wakope na wanapokopa wahakikishe wanabaki na nakala ya mkataba ili panapotokea changamoto mkataba huo uwalimde.

Kwa upande wake, Bw. Abonaventula Frederick, mkaazi wa Kasulu aliishukuru Wizara ya Fedha kwa Kutoa Elimu hiyo ambapo aliiomba Serikali kuendelea kutoa Elimu katika maeneo mengine kwani asilimia kubwa ya wananchi hawajui wapi wanatakiwa kuhifadhi fedha zao na wapi wanatakiwa wakope.

“Wananchi wengi hawajui wapi pakuhifadhi fedha zao na wengi wamekopa sehemu ambazo siyo sahihi hali ambayo imesababisha wauze mali zao ikiwemo mashamba ili walipe mikopo wanayodaiwa, hivyo wengi wakipata elimu hii wataelimika’. Alisema Bw. Frederick.

Naye Bi. Stephanie Fulmasi alisema kuwa wamepata elimu kupitia filamu ambayo imeandaliwa na Wizara hiyo na kupitia filamu hiyo wamejifunza namna gani wakina mama wanatakiwa kwenda kukopa sehemu sahihi na siyo kukopa sehemu yenye riba kubwa”. Amesema Bi. Stephanie.

Mafunzo ya elimu ya fedha yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Fedha yanalengo la kufikisha elimu na uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha.Kata zilizofikiwa mpaka sasa ni Buhingwe, Mnanila, Kinazi, Kasulu, Makere – VETA na Mvugwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *