RC MAKONDA AKABIDHI PIKIPIKI 50 NA GARI KWA JESHI LA POLISI

0

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameitaka Jamii ya Arusha kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani yote anayoyafanya mkoani Arusha yanatokana na maelekezo na uwezeshaji kutoka kwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Makonda ametoa wito huo leo Ijumaa Mei 31, 2024 wakati akikabidhi pikipiki 50 zenye thamani ya Milioni 145 zilizotolewa na Benki ya CRDB na NMB pamoja na kampuni ya vifaa vya umeme ya MCL pamoja na gari moja aina ya Fortuner lenye thamani ya Milioni 60 lililotolewa na Kamati ya Ulinzi na usalama mkoa wa Arusha.

Kando ya kuwashukuru wadau hao waliojitolea vitendeakazi hivyo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameahidi pia kutafuta magari mengine 50 kwa Jeshi hilo la Polisi badala ya magari 20 ya awali ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kutimiza maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuukuza utalii wa Mkoa wa Arusha kwa kuimarisha sekta mtambuka zinazohusiana na Utalii.

Wakati wa hotuba yake Mhe. Makonda na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo wametuma salamu kwa wahalifu wa Mkoa wa Arusha na kuwataka kuacha vitendo hivyo kabla ya hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao,wakionya wazazi kutoa tahadhari kwa watoto wao wanaojihusisha na uhalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha pia amelitaka Jeshi la Polisi Arusha kuimarisha kitengo chake cha Intelejensia ili kujenga heshima ya Jeshi la Polisi kwa kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu kabla ya wahalifu kusababisha madhara kwa jamii ya Arusha.

Aidha Mhe. Makonda pia amelitaka Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kuachana na matumizi ya karatasi na badala yake watambulishe mfumo wa TEHAMA kwenye vituo vyake vya Polisi ili kuweza kutunza rekodi za matukio ya uhalifu na wahalifu na kuwezesha vituo vya Polisi kuweza kusomana na makao makuu ya Polisi Mkoani Arusha.

Mhe. Mkuu wa Mkoa kadhalika amewataka pia wananchi wa Arusha kushiriki kikamilifu kwenye suala la ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *