DCEA WATOA ELIMU KWA ZAIDI YA WANAFUNZI 1500 JUU YA MADHARA YA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

0

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kati (DCEA) wakishirikiana na Afisa waTAKUKURU Mkoani Dodoma, Leo tarehe 31/5/2024 wametoa elimu kwa zaidi ya wanafunzi 1500 ,juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na elimu juu ya Kuzuia na kupambana na Rushwa katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo mkoani Dodoma.

Akifungua mafunzo hayo chuoni hapo, Kaimu Kamishna Msaidizi kanda ya kati kwa niaba ya Kamishna Jenerali Aretas J Lyimo, amewataka wanafunzi kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kwani sheria ziko wazi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya haitafumbia macho kwa yeyote atakayejihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, biashara, uzalishaji,usafirishaji,na ufadhili wa dawa za kulevya kwa namna yoyote ile kwani sheria itachukua mkondo wake.

Aidha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kanda ya Kati ,imebaini uwepo wa viashiria vya biashara za dawa za kulevya pamoja na matumizi ya dawa hizo ikiwemo bangi jirani na Taasisi za Elimu mkoani Dodoma na kuwataka wasimamizi wa Taasisi hizo wakiwemo walimu kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za wahusika wa matukio hayo kwa kupiga namba 119 ambayo ni bure.

Profesa Magreth Busheshe Naibu Mkuu wa Chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 6,000 akijihusisha katika masuala ya Taaluma, Tafiti na Ushauri, ameishukuru Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kati,Kwa jinsi walivyoweza kutoa elimu ya madhara ya matumizi ya Dawa za kulevya kwa wanachuo wa Hombolo na kusema kuwa, elimu iliyotolewa itawasaidia sana vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kama bangi na mirungi.

Kwa upande wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Hombolo, wameishukuru Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kupatiwa elimu na kuahidi kuwa Wazalendo katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *