WANAFUNZI 188,787 WACHAGULIWA KIDATO CHA TANO NA VYUO VYA KATI

0

Wanafunzi 188,787 waliokidhi vigezo wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 812 wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya kati nchini kwa mwaka 2024.

Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka shule za Serikali, zisizo za Serikali na watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Haya yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa wakati wa kuzungumzia uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi.

Amesema  Uchaguzi  huo umefanyika kwa kuzingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Mtaala ulioboreshwa.

“Hivyo, Wanafunzi wote 188,787, waliokidhi vigezo wakiwemo wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 812 wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo vya kati katika fani mbalimbali.”

Mchengerwa alisema wanafunzi 131,986 wakiwemo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano 622 zikiwemo shule mpya 82 zinazoanza mwaka huu.

Alisema kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 1,462 wakiwemo wasichana 669 na wavulana 793 wamepangwa katika shule za sekondari 8 zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls.

Pia wanafunzi 6,576 wakiwemo wasichana 3,449 na wavulana 3,127 wamepangwa katika Shule za Sekondari za Kutwa za Kidato cha Tano,

Alisema pia wanafunzi 123,948 wakiwemo wasichana 62,636 na wavulana 61,312 wamepangiwa katika shule za Sekondari za Bweni za Kitaifa za Kidato cha Tano.

Aidha, Mchengerwa alisema wanafunzi 56,801 wakiwemo wasichana 17,332 na wavulana 39,469 wamepangiwa kujiunga kwenye kozi na fani mbalimbali za Stashahada katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Alisema kati ya hao wanafunzi 2,107 wakiwemo wasichana 804 na wavulana 1,303 wamechaguliwa kujiunga katika Vyuo vinne vya Elimu ya Ufundi ambavyo ni Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Usimamizi na Maendeleo ya Maji (WDMI).

Pia wanafunzi 2,019 wakiwemo wasichana 1,011 na wavulana 1,008 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Afya ngazi ya Stashahada.

Alisema pia wanafunzi 52,675 wakiwemo wasichana 15,717 na wavulana 37,158 wamechaguliwa kujiunga kwenye kozi mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Ufugaji, Utawala, Biashara na zinginezo za Stashahada katika Vyuo Elimu ya Ufundi mbalimbali nchini.

Aidha, Mchengerwa alisema Serikali imehakikisha wanafunzi wote wenye sifa wamepata nafasi kwenye shule na vyuo vya elimu ya ufundi.

“Hili ni lengo la Serikali kuendelea kutoa huduma kwa Watanzania wote na haswa wakati huu tunaotoa elimu bila ada.”

“Nipende kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha miundombinu ya Elimu inapatikana ambayo imewezesha wanafunzi wote waliokuwa na sifa kuchaguliwa kidato cha tano na vyuo.”

Aidha, Mchengerwa alisema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza Julai Mosi mwaka huu na kuwataka wanafunzi waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kaunza kuripoti shuleni kuanzia Juni 30 mwaka huu.

“Siku ya mwisho ya kuripoti shule walizopangiwa itakuwa tarehe 14 Julai mwaka 2024.”

Mchengerwa alisema kwa wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika vyuo walivyopangwa.
“Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika shule, hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kutokana na ukosefu wa nafasi.”

“Wazazi na walezi wote tuendelee na moyo huu wa kusimamia na kufuatilia maendeleo ya watoto ikiwemo kuwalea katika malezi na maadili mema ili wawe raia wema na wanaotegemewa na Taifa letu.”

Mchengerwa pia amewataka wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi kuendelea kufanya bidii katika kujifunza ili waweze kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya elimu ya juu baada ya kuhitimu Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu ya Ufundi.

Mchengerwa pia amewataka wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila Tarafa inatekelezwa.

“Hii itawezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.”

“Upanuzi na ujenzi wa Shule Mpya za Kidato cha Tano na Sita uendelee kufanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza tahasusi za masomo ya Sayansi. Mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zake ili kuwapunguzia wazazi na walezi na wanafunzi gharama za usafiri kwenda shule za mbali.”

Watahiniwa 572,359 walifanya mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2023, watahiniwa wa shule walikuwa 543,332 na wa Kujitegemea ni 29,027.

Aidha, ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja, unaonesha kuwa watahiniwa 197,426 sawa na asilimia 37.42 walipata ufaulu wa Daraja la I – III, hali inayoonesha kuwa ufaulu wa watahiniwa wa mwaka 2023 umeongezeka kwa asilimia 0.47 ikilinganishwa na ufaulu wa Daraja la I – III wa watahiniwa 192,348 asilimia 36.95 wa mwaka 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *