BUNGE LAPITISHA BAJETI WIZARA YA UJENZI KWA ASILIMIA 100

0


Kwa kauli moja Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya ujenzi ya Shilingi trilioni 1.77 kwa asilimia 100 ambayo inakwenda kutekeleza vipaumbele tisa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja, vivuko, mizani na ukamilishaji viwanja vikubwa vya ndege.

Jana Mei 29,2024 Waziri Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliwasilisha makadirio ya bajeti ya kiasi hicho kwa mwaka 2024/25 ambapo kati ya fedha hizo, Sh bilioni 81.4 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. Trilioni 1.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwenye wasilisho lake, Waziri Bashungwa alisema katika mwaka huo wa fedha, Wizara inatarajia kutekeleza Mpango na Bajeti kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).

Michango ya wabunge ilionyesha mapema kuwa bajeti hiyo ingepitishwa kwa kishindo kwani wabunge wengi wakiwemo wa vyama vya upinzani walipongeza utendaji kazi wa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wengine huku wakilalamikia upungufu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara.

Kabla Waziri Bashungwa hajahitimisha, alisimama Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba ambaye alikiri kuwa Wizara ya Ujenzi imetengewa kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na majukumu makubwa waliyonayo na kusema Serikali imeliona na watakwenda kuongeza kiwango hicho kupitia mpango maalumu.

Akijibu hoja za wabunge, Waziri Bashungwa amesema fedha yoyote itakayopelekwa Wizara ya Ujenzi itatumiwa kwa malengo ya kuwasaidia Watanzania kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na Mvua na kuwa hakutakuwa na ukwanguaji wa Barabara ambao mwisho wake hautakuwa na tija.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo, kunatoa fursa kwa Wizara ya Ujenzi kuanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Mpango Mkakati wa Wizara (2021/22 – 2025/26), Ahadi za Viongozi Wakuu, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *