WAZIRI MAVUNDE ASISITIZA KIPAUMBELE CHA SERIKALI KATIKA UONGEZAJI THAMANI MADINI
Katika kuhakikisha rasilimali madini ambazo nchi ya Tanzania imejaliwa na Mwenyezi Mungu zinawanufaisha watanzania , Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha madini yote yanaongezwa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Hayo yalibainishwa Mei 16, 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam aliposhiriki hafla ya kuadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa Kampuni ya PULA Group.
“Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi wasaidizi wake kuhakikisha tunasimamia uongezaji thamani wa rasilimali madini ili yanufaishe watanzania wengi zaidi ndiyo sababu tunasimama kifua mbele kutekeleza maagizo hayo ya Serikali kwa maslahi mapana ya Nchi yetu” alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa, ni dhamira ya Serikali kuona kwamba madini yote yanasafirishwa yakiwa yameongezwa thamani sababu ambayo imepelekea Wizara kuweka mkakati ambao pamoja na kuvutia uwekezaji, umeweka sharti la uwekezaji huo uendane samamba na uongezaji thamani wa madini yatakayochimbwa.
Vilevile, Mhe Mavunde alitoa rai kwa wawekezaji wengi kuchamgamkia fursa ya uwekezaji kutokana na nchi ya Tanzania kubarikiwa madini ya aina nyingi, ikiwemo mazingira mazuri ya uwekezaji na miundombinu ya kisasa ambayo yanarahisisha uwekezaji wa aina yeyote katika sekta ya madini.
Akisisitiza kuhusu nafasi ya Tanzania katika mwelekeo wa dunia kwenye Nishati safi, Waziri Mavunde alieleza kuwa kama nchi ipo tayari kupokea wawekezaji katika madini mkakati na muhimu ambayo imejiwekea utaratibu ambao utawezesha kuyaongeza thamani hapa nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.
“Ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kwenye sekta ya madini ambapo, tunahitaji betri za kufungwa kwenye magari ya umeme zitengenezwe hapa nchini Tanzania na kupelekwa kufungwa kwenye magari moja kwa moja popote pale duniani”, alibainisha Mhe. Mavunde.
Awali, akitoa salamu za ubalozi, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Michael Battle alieleza kuwa dunia kwa sasa imeweka kipaumbele katika nishati safi, ambayo inatokana na madini muhimu na mkakati, na hivyo kutoa wito kwa Tanzania kuwalazimisha na kuwaomba wawekezaji wote watakaofika kwenye sekta ya madini sharti waongeze thamani hapa hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya PULA, Balozi Charles Stith alibainisha kwamba hakujiuliza mara mbili kuleta uwekezaji nchini Tanzania kutokana na kama nchi kubarikiwa uongozi thabiti na imara unaovutia na kulinda maslahi ya wawekezaji na kuongeza kuwa PULA inakwenda kuifanyaTanzania kama kitovu katika uwekezaji inaokwenda kupanua katika nchi zingine jirani kama Malawi .