WAZIRI MAVUNDE ASISITIZA KIPAUMBELE CHA SERIKALI KATIKA UONGEZAJI THAMANI MADINI

0

-Akaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha bidhaa zitokanazo na madini

-Viwanda vya kuzalisha malighafi ya betri za magari ya umeme kujengwa Kahama,Shinyanga

Katika kuhakikisha rasilimali madini ambazo tumejaaliwa na Mwenyezi Mungu zinawanufaisha watanzania, Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha madini yote yanaongezwa thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Ameyasema hayo jana tarehe 16 Mei, 2024 katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam aliposhiriki hafla ya kuadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa Kampuni ya PULA Group.

“Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi wasaidizi wake kuhakikisha tunasimamia uongezaji thamani wa rasilimali madini ili yanufaishe watanzania wengi zaidi. Na ndiyo maana tunasimama kifua mbele kutekeleza maagizo hayo ya Serikali kwa maslahi mapana ya Nchi yetu”

“Ni dhamira ya Serikali kuona kwamba madini yote yanasafirishwa yakiwa yameongezwa thamani. Na ndiyo maana tumeweka mkakati ambao pamoja na kuvutia uwekezaji, tumeweka sharti la uwekezaji huo uendane samamba na uongezaji thamani wa madini yatakayochimbwa”, alisisitiza Mhe. Mavunde.

Vilevile, Mhe. Mavunde alitoa rai kwa wawekezaji wengi kuchamgamkia fursa ya uwekezaji kwani Nchi yetu imejaaliwa madini ya aina nyingi, mazingira mazuri ya uwekezaji na miundombinu ya kisasa ambayo yanarahisisha uwekezaji wa aina yeyote katika sekta ya madini.

Aidha, akisisitiza juu ya nafasi ya Tanzania katika muelekeo wa dunia kwenye Nishati safi, Waziri Mavunde alieleza kuwa kama Nchi ipo tayari kupokea wawekezaji katika madini mkakati na muhimu ambayo tumejiwekea utaratibu ambao utawezesha kuyaongeza thamani hapa nchini kabla hayajasafirishwa nje ya nchi.

“Ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita kwenye sekta ya madini ambapo, tunahitaji betri za kufungwa kwenye magari ya umeme zitengenezwe hapa nchini Tanzania na kupelekwa kufungwa kwenye magari moja kwa moja popote pale duniani”, alibainisha mhe. Mavunde.

Awali, akitoa salamu za ubalozi, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, *Balozi Dkt. Michael Anthony Battle alieleza kuwa dunia kwa sasa imeweka kipaumbele katika nishati safi, ambayo inatokana na madini muhimu na mkakati, na kutoa wito kwa Tanzania kuwalazimisha na kuwaomba wawekezaji wote watakaofika kwenye sekta ya madini sharti waongeze thamani hapa hapa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya PULA, Balozi Charles Stith alibainisha kwamba hakujiuliza mara mbili kuleta uwekezaji nchini Tanzania kutokana na kama nchi kubarikiwa uongozi thabiti na imara unaovutia na kulinda maslahi ya wawekezaji na kuongeza kuwa PULA inakwenda kuifanyaTanzania kama kitovu katika uwekezaji inaokwenda kupanua katika nchi zingine jirani kama Malawi n.k.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *