SERIKALI KUNUNUA MITAMBO KUMI YA UCHORONGAJI KWA AJILI YA WACHIMBAJI WADOGO
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imepanga kununua mitambo mingine 10 ya uchorongaji kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo nchini.
Hayo yamesemwa leo 17 Mei, 2024 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde aliposhiriki zoezi la kuwakabidhi leseni Chama cha Wanawake Wachimbaji Mkoani Simiyu (TAWOMA) katika Kata ya Dutwa Wilayani Bariadi.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha za kuongeza mitambo mingine 10 ya uchorongaji kupitia STAMICO na ametuelekeza kuwa mitambo hiyo ikifika nchini Mwezi Agosti au Septemba, 2024 mitambo 2 tuiweke mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo wanawake na vijana” amesema Waziri Mavunde
Ameongeza kwamba ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwawezesha wachimbaji madogo kwa kuwapatia vifaa na kuimarisha shughuli zao ili ziwanufaishe watanzania.
Pia, Waziri Mavunde amwmwagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Simiyu, Bw. Mayigi Makolobela kusimamia vijana na wanawake ili waunde vikundi, ili katika maeneo yanayorejeshwa Serikalini kwa zoezi la ufutaji wa leseni vikundi hivyo vipatiwe maeneo ya uchimbaji.
Akisoma risala kwa niaba ya Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA) mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa TAWOMA Taifa, Bi. Semeni Malale ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuwawezesha wachimbaji wanawake nchini kuendesha shughuli zao na pia kumshukuru Ndg Emmanuel Silanga”Gungu” kwa kutoa Leseni hiyo kwa wakina mama wa Mkoa wa Simiyu.
Pia, panoja na mambo mengine, Bi. Semeni ametoa wito kwa wanawake wenzake kuchangamkia fursa hiyo ya uchimbaji baada ya kupokea leseni hiyo, huku akiiomba Serikali kuendelea kusaidia baadhi ya changamoto katika eneo la uchimbaji la Dutwa ikiwemo maji na barabara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Dkt. Yahaya Nawanda ameishukuru Serikali kwa namna inavyosimamia sekta ya madini, na kuahidi kwamba ataendelea kutoa ushirikiano kwa akina mama na vijana wachimbaji madini ili shughuli zao ziendelee kuwanufaisha na kuchangia katika ustawi wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu.
Akijibu changamoto za TAWOMA katika eneo la Dutwa, Mhe. Dkt. Nawanda amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga kuhakikisha anasimamia suala la kuboresha barabara na kuleta maji katika eneo hilo la uchimbaji, kwani Serikali imeshaleta zaidi ya bilioni 4 Mkoani Simiyu kwa ajili ya uboreshaji barabara na mtandao wa maji.