DAFTARI LA WAPIGA KURA KUANZA KUBORESHWA JULAI MWAKA HUU
Uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Unguja, Zanzibar, leo tarehe 15 Mei, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema kuwa zoezi hilo litakapokamilika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638.
“Kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hili ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.
Kuhusu idadi ya vituo, Jaji Mwambegele ameseama Tume ilifanya uhakiki wa vituo vya kuandikishia wapiga kura mwaka 2023 ambapo baada ya zoezi hilo iliamuliwa kuwa vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa Daftari ni 40,126.
“Kabla ya uhakiki huo wa vituo, kulikuwa na vituo 37,814 ambavyo vilitumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2019/2020. Baada ya zoezi hilo la uhakiki, jumla ya vituo 40,126 vitatumika kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari mwaka 2024/2025 ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.
Amefafanua kuwa siku ya uzinduzi ndiyo siku ambayo pia uboreshaji utaanza katika mkoa wa Kigoma na kuendelea katika mikoa mingine ya Katavi, Rukwa na Tabora.
“Kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba. Aidha, zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema kuwa zoezi hilo litahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 pamoja na wale ambao hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote.
“Zoezi hilo pia litatoa fursa kwa wapiga kura waliandikishwa awali na ambao wamehama kutoka mkoa au wilaya moja kwenda nyingine waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurebisha taarifa zao yakiwemo majina….,” amesema Jaji Mwambegele.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa zoezi hilo la uboreshaji wa Daftari litahusisha pia kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza au kadi zao kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
“Kwa upande wa Zanzibar uboreshaji wa Daftari utamhusu mtu yeyote aliyepo Zanzibar ambaye hana sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar lakini ana sifa ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema Tume imefanya ununuzi wa vifaa vya uandikishaji ikiwemo ununuzi wa BVR Kits 6,000 zinazotumia vishikwambi kuchukua taarifa za wapiga kura ikiwemo picha, saini na alama za vidole.
“Tofauti na mashine za BVR zilizotumika katika uboreshaji wa mwaka 2015 na 2020 zilizokuwa na uzito wa kilo 35, BVR Kits za awamu hii ni nyepesi zenye uzito wa kilo 18 ambazo zitaweza kubebeka kwa urahisi,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesema, Tume imeanzisha mfumo wa uboreshaji kwa njia ya mtandao uitwao Online Voters Registration System (OVRS) ambao utamuwezesha mpiga kura aliyemo kwenye Daftari kuanzisha mchakato wa awali wa kuboresha taarifa zake kwa njia ya mtandao kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta.
“Baada ya kukamilisha mchakato kwa njia ya mtandao mpiga kura atalazimika kufika kituo cha kuandikisha wapiga kura ili kukamilisha mchakato na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura,” amesema Jaji Mwambegele.