WIZARA YA MAJI KUANZA KUTEKELEZA MKAKATI WA GRIDI YA TAIFA YA MAJI

0

Waziri wa Maji Nchini Mhe. Jumaa Aweso amesema Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza utekelezaji wa mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji kwa kutumia vyanzo vikubwa vya maji vya uhakika ikiwemo maziwa, mito mabwawa kwa ajili ya kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayana vyanzo vya uhakika.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 Bungeni Dodoma leo tarehe 9 Mei, 2024 , Waziri Aweso ametolea mfano wa utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji ambapo amesema mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria umenufaisha miji ya Kahama, Shinyanga, Tinde, Nzega, Tabora, Igunga na Shelui pamoja na vijiji vilivyopo ndani ya kilomita 12 kutoka kwenye bomba kuu.

Pia ametolea mfano mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka kwenye mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ambapo upo kwenye hatua ya usanifu.

Vilevile, Waziri Aweso amesema wizara hiyo imeanza utekelezaji wa miradi ya maji ya kimkakati ikiwemo mabwawa ya Kidunda na Farkwa pamoja na Mradi wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi – Simiyu.

Aidha, Aweso ameongeza kuwa Wizara imefanikiwa kukwamua miradi 157 kati ya miradi 177 ya maji vijijini iliyokuwa na changamoto ya kutokukamilika kwa muda mrefu.

Sambamba na hayo, Waziri Aweso amebainisha kuwa Wizara hiyo imefanikisha kuanzishwa kwa Consultancy Bureau katika Chuo Cha Maji inayosaidia kutoa huduma za ushauri elekezi kwenye sekta ya maji na sekta nyinginezi ikiwa ni pamoja na uandaaji na usimamizi wa miradi pamoja na kuwajengea uwezo Vijana wanaohitimu masomo na kusaidia kuongeza mapato ya Taasisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *