MCHENGERWA ATAKA HEWA UKAA KUWA CHANZO KIPYA CHA MAPATO YA HALMASHAURI

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao maeneo yao kuna misitu ya asili kuhakikisha wanaanzisha biashara ya hewa ukaa kama chanzo kipya cha mapato.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga kikao cha siku tatu na Wakurugenzi hao kilichofanyika shule ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo kibaha mkoani Pwani.

Amesema biashara ya kaboni ni biashara mpya na inafanya vizuri sana kwenye baadhi ya Halmashauri kama vile Tanganyika na ni chanzo kizuri cha mapato na cha uhakika.

“Sasa nizitake halmashauri zingine zote zenye misitu kuhakikisha wanaaza biashara hii mara moja, ninawapa mwezi mmoja Halmashauri zote zenye Misitu muende mkajifunze kwa Halmashauri ya Tanganyika ambao wameshafika mbali kwenye Biashara hii na kwa mwala wanapata Sh.Bilioni 14 ambazo zinasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo na nyie mkajifunze muone namna ya kuanza biashara hii ili kuongeza mapato ya Halmashauri.”

“Mtakumbuka kuwa wiki mbili zilizopita wakati nafungua Mkutano wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania niliwaelekeza kila Mkurugenzi kuhakikisha ameanzisha vyanzo vipya viwili vya mapato sasa niwape chanzo cha kuanza nacho ni hiki cha hewa ukaa,”amesema.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza Wakurugenzi hao kwenda kusimamia ajenda ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kutumia mashine za kieletroniki pamoja na matumizi sahihi ya
mapato hayo hususan ni kwenye miradi ya maendeleo.

“Mapato na damu ya maendeleo bila mapato hakuna maendeleo, bado hamfanyi vizuri kwenye eneo hili, nendeni mkakusanye mapato kikamilifu na mtumie mifumo ipasavyo katika zoezi zima la ukusanyaji, matumizi ya mifumo ya kielektroniki yameonyesha mafanikio makubwa na ufanisi katika ukusanyaji wa fedha za Serikali,”amesema.

Awali, akisoma taarifa ya Wakurugenzi, Mwenyekiti wa Wakurugenzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuona umuhimu wa kuitisha kikao hicho na kuahidi watakwenda kufanya kazi kama walivyoaminiwa na Mhe. Rais Dkt. Salia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *