ZAIDI YA BILIONI 11 ZIMELIPWA KAMA KIFUATA JASHO NA MACHOZI
Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma.
Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 11,085,850,400 kama kifuta jasho na kifuta machozi kuanzia Mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Machi, 2024, kwa wananchi waliothirika na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.
Hayo yamebainika wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula akijibu swali la Mhe. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka (Mb) aliyetaka kujua, katika kipindi cha 2017 – 2022 ni kiasi gani cha fedha kimelipwa kama kifuta jasho kwa uharibifu wa mazao na watu kuuliwa na Tembo.
Aidha Mhe. Kitandula amebainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii tayari imezifanyia marekebisho kanuni za kifuta jasho na machozi, na kwamba kwasasa ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na Wizara ya Fedha ili kupata ridhaa ya matumizi ya viwango vipya vya fidia kwakua viwango vilivyopo sasa vimepitwa na wakati.
Hata hivyo Mhe. Kitandula aliongeza kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kulipa fedha hizo kwa wakati mara pale inapopata taarifa kutoka kwenye Halmashauri za wilaya na mchakato wa tathimini kufanyika ili kujua gharama halisi ya fedha inayotakiwa kulipwa.
Mhe. Kitandula alisema kuwa serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kujenga vituo vya askari kwenye makazi ya wananchi ili kuwasogeza askari karibu na maeneo yenye changamoto.
“moja ya jitahada zilizofanywa na Serikali ni kujenga vizimba vya kuzuia mamba wasidhuru wananchi wanapotumia maji ya mito au maziwa” alisema Mhe. Kitandula
Vilevile serikali imeandaa mfumo wa kielektroniki ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na utunzaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu lakini pia imeweka namba maalum za simu kwenye vituo vya kanda za kiutendaji za taasisi za uhifadhi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.