MAHIMBALI APOKEA TAARIFA MAANDALIZI WIKI YA MADINI KUTOKA FEMATA
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amekutana na kuzungumza katika kikao kifupi na Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Madini, Maonesho na Kongamano la Wachimbaji Madini Tanzania.
Kikao hicho kimefanyika leo Mei 07, 2024 ofisini kwake Jijini Dodoma ambapo Kamati hiyo imefika ofisini hapo ili kutoa taarifa ya maandalizi ya shughuli hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Mahimbali ameipokea taarifa ya maandalizi ya shughuli hiyo na kuwapongeza wajumbe wa Kamati hiyo kwa maandalizi ya shughuli hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) kwa kushirikiana na Wizara ya Madini.
Aidha, Wiki ya Madini, Maonesho na Kongamano la Wachimbaji Madini Tanzania linatarajiwa kufanyika June 20 mpaka 27, 2024 Jijini Dodoma ambapo Wachimbaji Wadogo, wa Kati, Wakubwa na Wadau wote wa Sekta ya Madini watashiriki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Peter Kabepela amesema lengo la Wiki ya Madini, Maonesho na Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania ni kutoa Dira ya FEMATA katika Mwaka wa Fedha 2024/25 kwa wadau mbalimbali wa Sekta hiyo.