HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWA MWAKA 2024/25

0

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

MUHTASARI WA HOTUBA YA BAJETI YA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA PROF. ADOLF F. MKENDA (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2024/25

DODOMA                                                                         MEI, 2024 

A.          UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, Baada ya Bunge lako Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo iliyochambua makadirio ya mapato na matumizi ya FUNGU 46 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na FUNGU 18 – Tume ya Taifa ya UNESCO, ninaomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa mwaka wa fedha 2023/24. Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25.
  2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kumshukuru MwenyeziMungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana leo kujadili utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 na makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Taifa ya UNESCO kwa mwaka wa fedha 2024/25.
  3. Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Bunge lako Tukufu, ndugu, jamaa, na Watanzania wote kwa kuondokewa na kiongozi wetu mpendwa Hayati Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika tutaendelea kumuenzi kwa mchango wake mkubwa katika mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kielimu hususan kwa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu nchini.
  4. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninaomba kumpa pole Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa kuondokewa na Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atakumbukwa kwa uchapakazi na umahiri wake katika usimamizi wa kazi za Serikali ikiwemo uanzishaji wa Shule za Sekondari za Kata zilizoongeza fursa ya elimu ya sekondari nchini.
  5. Mheshimiwa Spika, pia naomba kuungana na wabunge wenzangu waliotangulia kutoa pole kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil (Mb) aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani Zanzibar ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo.
  6. Mheshimiwa Spika, ninaomba kuhitimisha salamu zangu za pole kwa kutoa pole kwa Watanzania wote waliopoteza ndugu na jamaa na kupoteza au kuharibikiwa na mali kutokana athari za mvua kubwa zinazoendelea nchini. Mwenyezi Mungu awape marehemu pumziko la milele, Amina! Aidha, tunamwomba Mwenyezi Mungu awajalie uponyaji majeruhi wote ili waweze kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa.
  7. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutimiza miaka mitatu ya uongozi ulio mahiri na wenye weledi mkubwa. Katika kipindi cha miaka mitatu, Mheshimiwa Rais ametuongoza katika kupata mafanikio makubwa nchini ikiwemo mageuzi katika mfumo wa elimu na mafunzo yanayolenga kuandaa nguvu kazi yenye maarifa, stadi na mtazamo chanya katika kuleta maendeleo endelevu ya Taifa letu. Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Rais kwa miongozo na maelekezo yake yaliyotusaidia katika kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na kufanya marekebisho kwenye mitaala ili kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira ya nchi na soko la ajira.
  8. Mheshimiwa Spika, aidha, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini mimi pamoja na Mheshimiwa Omary Juma Kipanga (Mb) Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuongoza Wizara hii.
  9. Mheshimiwa Spika, vilevile, ninaomba kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb) Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa uongozi wao mahiri katika kuliongoza Taifa letu.
  10. Mheshimiwa Spika, ninapenda kukupongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani; Mwanamke wa tatu kushika nafasi hiyo duniani na wa kwanza kutoka Afrika. Vilevile, ninakupongeza Mheshimiwa Spika pamoja na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa umahiri mkubwa. Aidha, natumia nafasi hii kuwapongeza wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Dkt. Joseph Mhagama Mbunge wa Madaba na Mheshimiwa Deo Mwanyika Mbunge wa Njombe Mjini kwa umakini wao katika kuliongoza bunge lako Tukufu.
  11. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Zainabu Athuman Katimba (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
  12. Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru kwa namna ya pekee Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Makamu Mwenyekiti Musa Ramadhani Simma na wajumbe wote wa Kamati. Aidha, naomba niwashukuru kwa kupokea, kuchambua na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2023/24 na kuishauri vema Wizara kuhusu Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2024/25. Natambua na kuthamini sana mchango wa Kamati katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inachangia katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano 2021/22 – 2025/26 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 kwa kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi, maarifa na stadi zitakazowezesha kujenga uchumi shindani wa viwanda na kuendelea kustawisha maisha ya kila Mtanzania, kutokomeza umasikini na kuhakikisha kuwa Taifa linafikia uchumi wa kati.
  13. Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Rombo kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Aidha, kwa namna ya pekee napenda kuishukuru familia yangu hasa mke wangu mpendwa Beatrice kwa kuendelea kuwa karibu yangu na kunitia moyo na kuniwezesha kufanya kazi kwa juhudi na ari kubwa.
  14. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi, naomba sasa nitoe taarifa ya utelekezaji wa majukumu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, na Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.


B.       UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2023/24

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI

  1. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/24 Bunge lako Tukufu liliidhinisha kiasi cha Shilingi 1,675,753,327,000.00 kwa ajili ya FUNGU 46 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Shilingi 537,880,762,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 1,137,872,565,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aidha, kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO – FUNGU 18 Wizara iliidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,733,888,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo yanajumuisha Shilingi 1,124,980,000.00 za Mishahara na Shilingi 1,608,908,000.00 za Matumizi Mengineyo.

Ukusanyaji wa Maduhuli

  1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/24 Wizara kupitia FUNGU 46 ilitarajia kukusanya maduhuli yenye thamani ya Shilingi 679,362,572,548.64 ambapo kiasi cha Shilingi 11,660,695,000.00 kilipangwa kukusanywa na idara na vitengo na Shilingi 667,701,877,548.64 zilipangwa kukusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara. Vyanzo vya maduhuli hayo ni kutokana na ada, malipo ya ushauri elekezi, huduma za Uthibiti Ubora wa Shule na utoaji wa huduma mbalimbali.
  2. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 15, 2024 Wizara imekusanya Shilingi 397,598,746,452.42 sawa na asilimia 59 ya makadirio ambapo Shilingi 11,072,869,322.29 zimekusanywa na idara na vitengo na Shilingi 386,525,877,130.13 zimekusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara.

Matumizi ya Kawaida

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara pamoja na taasisi zake iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 537,880,762,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Matumizi ya mishahara ni Shilingi 500,957,569,000.00 (idara na vitengo Shilingi 83,200,218,000.00 na Taasisi ni Shilingi 417,757,351,000.00) na Matumizi Mengineyo Shilingi 36,923,193,000.00 (idara na vitengo ni Shilingi 26,416,806,658.00 na Taasisi Shilingi 10,506,386,342.00).
  2. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 15, 2024, Wizara imepokea Jumla ya Shilingi 405,900,247,712.40 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, kupitia Fungu 46 sawa na asilimia 75 ya fedha za Matumizi ya Kawaida zilizoidhinishwa. Aidha, kupitia Tume ya UNESCO – Fungu 18 Wizara imepokea jumla ya Shilingi 1,906,916,317.62 sawa na asilimia 70 ya fedha ya matumizi ya kawaida iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Miradi ya Maendeleo

  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, Wizara pamoja na taasisi zake iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,137,872,565,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo fedha za ndani ni Shilingi 979,083,678,000.00 na fedha za nje ni Shilingi 158,788,887,000.00.
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miradi ya maendeleo hadi kufikia Aprili 15, 2024, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 988,594,227,608.28 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 87 ya bajeti iliyotengwa. Kati ya Fedha hizo Shilingi 900,697,116,186.31 ni fedha za ndani na Shilingi 87,897,111,421.97 ni fedha za nje.

C.   TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA

  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitekeleza vipaumbele vitano ambavyo ni:
  • kukamilisha Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji wake kwa lengo la kuimarisha ujuzi kwa wahitimu;
  • kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali (ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) kwa sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi;
  • kuwezesha Ongezeko la fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu;
  • kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu; na
  • kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

a.            Kuhuisha Sera na Sheria, na Utoaji wa Miongozo ya Elimu na Mafunzo Nchini.

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na kuandaa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023. Vilevile, tumefanya mabadiliko makubwa na kuboresha mitaala ya elimu ya awali, elimu ya msingi na elimu ya sekondari, pamoja na mafunzo ya ualimu. Utekelezaji wa mitaala mipya imeanza kwa awamu kuanzia Januari 2024. Aidha, katika kuhakikisha mitaala inatekelezwa kwa ufanisi, Serikali imetoa Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2023 wenye kutoa mwongozo wa utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa ili kurahisisha utekelezaji wake. Uboreshaji wa sera na mitaala utaimarisha utoaji wa elimu na kuwezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo kupata elimu bora zaidi kitaaluma na pia yenye ujuzi na maarifa yenye kuendana na mipango ya nchi na mahitaji ya kitaaluma na ajira.
  2. Mheshimiwa Spika, ili mitaala iliyoboreshwa iweze kutekelezwa ipasavyo Serikali imewajengea uwezo walimu na wasimamizi kuhusu utekelezaji wa mitaala kama ifuatavyo:
  3. imetoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa kwa wawezeshaji 11,521 wa kitaifa ambao ni; walimu weledi wa darasa la awali, maafisa elimu kata, wathibiti ubora wa shule; na walimu weledi kutoka taasisi mama zinazomiliki shule zisizo za Serikali, wakuza mitaala na wakufunzi;
  4. imewajengea uwezo viongozi wa elimu 569 wakiwemo maafisa elimu wa mikoa, maafisa elimu msingi, maafisa elimu taaluma, maafisa elimu wa elimu maalum na wathibiti ubora wa shule kuhusu usimamizi na utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa;
  5. imetoa mafunzo kwa walimu 182,697 sawa na asilimia 81 ya walimu wa awali na msingi kuhusu mitaala iliyoboreshwa wakiwemo walimu 155,476 wa shule za Serikali, 26,301 wa shule zisizo za Serikali, na walimu 920 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum waliofundishwa kuhusu mitaala iliyoboreshwa na utoaji wa elimu jumuishi;
  6. imetoa mafunzo kuhusu Maudhui ya Ufundishaji wa Somo la English na Sayansi kwa walimu wa shule ya msingi 70,717 (shule za Serikali 69,872 na shule zisizo za Serikali 845);
  7. imetoa mafunzo ya walimu 346 (walimu wa shule za Serikali 147 na zisizo za Serikali 199) wa Kidato cha Kwanza Mkondo wa Amali katika shule 96 (shule za Serikali 28 na zisizo za Serikali 68) ambazo zimeteuliwa kuanza kutekeleza Mtaala wa Amali Mwaka 2024;
  8. imetoa mafunzo kwa walimu 428 wanaofundisha masomo ya Historia ya Tanzania na Maadili, English, Elimu ya Biashara na Hisabati katika shule 96 za sekondari zilizoteuliwa kutekeleza mtaala kwa kidato cha kwanza Mkondo wa Amali; na
  9. imechapa na kusambaza nakala 9,818,251 za mihtasari, vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu kwa mchanganuo ufuatao: nakala 509,582 za mihtasari na mitaala iliyoboreshwa wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari, nakala 8,074,326 za vitabu vya kiada vya kimacho kwa darasa la awali, darasa la I na la III, nakala 43,785 za vitabu vya maandishi yaliyokuzwa kwa darasa la awali, darasa la I na la III, nakala 6,990 za vitabu vya breli, nakala 1,183,568 za viongozi vya mwalimu na nakala za vitabu 6,900 vya masomo ya amali kwa kidato cha kwanza katika shule 96 (Serikali 28 na  zisizo za Serikali 68).
  10. Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa miongozo mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa Sera na Mitaala. Miongozo hiyo ni:
  11. Mwongozo wa Shule ya Nyumbani; Mwongozo wa Ziara ya Nyumbani; Mwongozo wa Ubainishaji na Upimaji wa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum, Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Elimu pamoja na Mwongozo wa Utoaji wa Huduma za Kielimu Maalum kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum ili kuimarisha utoaji wa elimu jumuishi nchini. Aidha, wanafunzi 429 wenye kiwango cha juu cha mahitaji maalum na changamoto ya afya wanafundishwa masomo mbalimbali na kupata huduma ya utengamao na uchechemuzi wakiwa nyumbani; na
  12. Mwongozo wa Utoaji wa Elimu ya Kujitegemea katika Shule za Awali, Msingi na Sekondari Tanzania Bara.

b.   Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Mafunzo ya Amali (Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi) kwa Shule za Sekondari na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

  • Mheshimiwa Spika, katika kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuboresha mafunzo yaufundi na mafunzo ya ufundi stadi Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imebainisha shule 96 za sekondari (shule za Serikali ni 28 na zisizo za Serikali ni 68) ambazo zimeanza kutekeleza mitaala ya amali mwaka 2024;
  • imekamilisha ujenzi wa vyuo 29 vya mafunzo ya ufundi na ufundi stadi kati ya hivyo 25 ni vya wilaya na vinne ni vya kiwango cha mkoa. Vyuo 25 vya VETA vya Wilaya vimeanza kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi. Aidha, Serikali imetoa vifaa vya kufundishia, mitambo na kompyuta 20 kwa kila chuo kwa lengo la kuimarisha mafunzo kwa vitendo;
  • imeanza ujenzi wa Vyuo 64 vya VETA vya Wilaya kikiwemo chuo cha VETA Chamwino ambapo ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 83. Kadhalika Serikali imejenga chuo cha VETA cha kiwango cha mkoa wa Songwe. Ujenzi huo unajumuisha majengo 18 kwa kila chuo cha Wilaya na majengo 25 kwa chuo cha Mkoa. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa karakana nne kwa ajili ya fani ya umeme, ufundi bomba, ujenzi na ufundi magari katika Chuo cha VETA cha Kihonda ambapo ujenzi umefikia asilimia 25. Aidha, imekamilisha ujenzi wa awamu wa kwanza ya Chuo cha Ufundi Dodoma chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 3000.
  • imekamilisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wa kike yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 436 katika Chuo cha Ufundi Arusha; ujenzi wa madarasa 10 yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,800 katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Pemba ambapo ujenzi umefikia asilimia 85 pamoja na hosteli mbili zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 768 kila moja katika Kampasi ya Karume Zanzibar ambapo ujenzi umefikia asilimia 49.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fursa za mafunzo ya amali kupitia vyuo vya Amali kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeongeza udahili katika vyuo vya elimu ya ufundi (technical education and training colleges) kutoka wanafunzi 171,581 (wanawake 93,684) mwaka 2022/23 hadi wanafunzi 235,804 (wanawake 114,079) mwaka 2023/24. Ongezeko hili linatokana na kuongezeka kwa idadi ya vyuo vya elimu ya ufundi kutoka vyuo 465 (visivyo vya Serikali 285) mwaka 2022/23 hadi vyuo 474 (visivyo vya Serikali 294) mwaka 2023/24; na
  • imeongeza uandikishaji wa wanachuo katika vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (vocational education and training colleges) kutoka wanafunzi 380,748 (wanawake 155,127) mwaka 2022/23 hadi wanafunzi 454,937 (wanawake 171,865) mwaka 2023/24. Ongezeko hili linatokana na kuongezeka kwa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi kutoka 687 (visivyo vya Serikali 563) mwaka 2022/23 hadi kufikia vyuo 830 (visivyo vya Serikali 705) mwaka 2023/24.
  • Mheshimiwa Spika, katika eneo la ithibati na uthibiti wa mafunzo ya amali (ufundi na mafunzo ya ufundi stadi), Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imesajili vyuo 29 katika bodi za masomo zifuatazo: Afya na Sayansi Shirikishi vyuo vinne; Biashara, Utalii na Mipango vyuo nane; Bodi ya Sayansi na Teknolojia Shirikishi vyuo vinne na vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi 13. Aidha, imetoa ithibati kwa vyuo 40 katika bodi za masomo zifuatazo: Afya na Sayansi Shirikishi vyuo 16; Biashara, Utalii na Mipango vyuo 17 na Sayansi na Teknolojia Shirikishi vyuo saba pamoja na programu 12 za ufundi na mafunzo ya ufundi stadi;
  • imetoa Namba za Uhakiki wa Tuzo (AVN) 57,158 kwa lengo la kuimarisha uhakiki wa taarifa mbalimbali za wahitimu wa stashahada wanaoendelea na Elimu ya Juu pamoja na kuviwezesha vyuo kuhakiki udahili unaofanywa na Tume ya Vyuo Vikuu;
  • imehakiki mitaala 117 kati ya 230 iliyoandaliwa na Vyuo vya Ufundi kwa lengo la kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wahitimu; na
  • imefanya ufuatiliaji na tathmini ya ubora wa elimu katika shule za Amali 96 na Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi 108 kati ya lengo la vyuo 400. Aidha, shule na vyuo vilipewa ushauri wa namna ya kuboresha utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Vyuo ambavyo havikukidhi vigezo vilichukuliwa hatua stahiki ikiwemo kuvisimamisha na/au kuvifutia usajili ili kuvipa nafasi ya kurekebisha mapungufu yaliyobainika.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi na Mashirika mbalimbali katika utoaji wa mafunzo kwa vitendo katika Vyuo vya Ufundi kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeendelea kushirikiana na taasisi na mashirika 22 kutoka sekta rasmi na kutoa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi 1,128 (wanawake 307) na walimu 23 (wanawake 3) kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wa mafunzo ya amali wanapata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa; na
  • imeanza utekelezaji wa Programu ya Integrated Training for Entrepreneurship Promotion (INTEP) katika kanda 7 (Dar es Salaam, Mashariki, Kaskazini, Ziwa, Kusini Magharibi, Magharibi na Kati) ambapo jumla ya wanufaika 2,101 (wanawake 1,483) sawa na asilimia 105 ya lengo walipatiwa mafunzo katika fani za ushonaji, kilimo, uvuvi, mama lishe, mapishi na ufugaji kupitia VETA.
  • Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha mafunzo kwa vitendo kupitia utaratibu wa uanagenzi kwa wanafunzi wa vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa kuwajengea uwezo walimu 16 na walezi 19 kuhusu utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi pacha. Aidha, imetoa mafunzo kwa wanafunzi 376 ambapo Programu ya Mafunzo ya Uanagenzi 195 (wanawake 87) na programu ya kukuza ajira na ujuzi kwa vijana 181 katika fani za umeme wa viwandani na nishati ya jua, ufundi vipuri, ufundi majokofu, na utayarishaji wa vyakula.

c.    Kuwezesha Ongezeko la Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu

  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetekeleza yafuatayo:
  • imewezesha ujenzi wa shule mpya za sekondari ngazi ya kata 228 na shule 26 za Sayansi za Wasichana za bweni za mikoa. Vilevile, imewezesha ujenzi wa shule mpya za msingi 302 nchi nzima;
  • imewezesha ujenzi wa madarasa 4,140, maabara 18, mabweni 119, matundu ya vyoo 21,237 na nyumba za walimu 285 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 456 katika shule za msingi na sekondari; na
  • imewezesha ukamilishaji wa ujenzi wa maboma ya vyumba vya madarasa 869, maabara za sayansi 132 na matundu ya vyoo 1,650 katika shule mbalimbali nchini.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fursa za elimu kwa kutoa ithibati kwa shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imesajili jumla ya shule 1,073 zilizoomba usajili na kukidhi vigezo ambapo; Shule za Awali Pekee 42 (zisizo za Serikali), Awali na Msingi 707 (zisizo za Serikali 187), na Sekondari 324 (zisizo za Serikali 26); na
  • imetoa vibali vya kuanzisha shule 251 mpya zilizokidhi vigezo kati ya shule 315 zilizoomba. Kati ya shule hizo, shule za awali pekee 31, awali na msingi 180 na sekondari 40.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ubora wa elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imefanya tathmini ya jumla ya asasi 7,418 zikiwemo asasi za Serikali 6,011 na zisizo za Serikali 1,407. Katika tathmini hiyo asasi zilizobainika kuwa na mapungufu zilipewa ushauri wa kitaalam na kitaaluma kwa ajili ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji; na
  • imefanya ufuatiliaji wa ushauri uliotolewa wakati wa tathmini ya jumla katika shule za msingi 1,750, sekondari 382 na chuo cha ualimu kimoja. Ufuatiliaji ulibaini mabadiliko chanya ya viwango vya ubora baada ya kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa katika tathmini ya jumla.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha fursa ya elimu ya ualimu kwa kusajili jumla ya wanachuo 23,331 (wanawake 11,224) ambapo katika vyuo vya ualimu vya Serikali wanachuo ni 23,162 na Visivyo vya Serikali wanachuo ni 169. Vilevile, imeendelea na ujenzi mpya wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda, Dakawa na Ngorongoro ambapo ujenzi wa vyuo hivyo umefikia asilimia 95.
  • Mheshimiwa Spika, umahiri wa walimu na wakufunzi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imetoa mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali 4,000 kuhusu ujuzi wa kufaragua zana za kufundishia na kujifunzia zinazotokana na rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao;
  • imetoa mafunzo kwa walezi na waangalizi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum 148 kuhusu namna ya kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na stadi za maisha ikiwemo ufugaji wa kuku na uanzishaji wa bustani ili waweze kujikimu.
  • imetoa mafunzo kwa walimu 80 wa shule za msingi na sekondari wasioona kuhusu namna ya kutumia vifaa vya kidijiti kama vile kompyuta katika kufundishia na kujifunzia; na
  • imetoa mafunzo ya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa washiriki 114 wakiwemo maafisa elimu wilaya na mikoa, maafisa ustawi wa jamii, maafisa wauguzi, maafisa taaluma wa mikoa, walimu wa elimu maalum, na maafisa elimu maalum wilaya katika mikoa mitano ambayo ni Tabora, Kigoma, Katavi, Kagera na Rukwa iliyokuwa chini ya wastani wa asilimia 50 ya uandikishaji wa watoto wenye mahitaji maalum.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi wa elimu ya awali, msingi, na sekondari ili kuimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeandaa moduli 12 za mafunzo kwa darasa la awali, I, na III kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watekelezaji wa mitaala mpya;
  • imeandaa mitaala nane na mihtasari 114 katika ngazi ya elimu ya awali, msingi (darasa I – VI), sekondari (kidato cha 1 – 4 na kidato cha 5 – 6) na ualimu (elimu ya Awali, msingi, elimu maalum na mafunzo ya ualimu wa karakana);
  • imekamilisha kutafsiri mihtasari 23 ya elimu ya ualimu na aina 93 za vitabu vya mitaala iliyoboreshwa wa darasa la elimu ya awali, darasa la I na III, na kidato cha kwanza mkondo wa amali;
  • imeandaa aina 19 ya vitabu vya darasa la awali, I na III katika maandishi makubwa kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na aina 19 nyingine katika maandishi ya breli kwa ajili ya wanafunzi wasioona na aina 31 za vitabu vya kiada kwa kidato cha 5 na 6;
  • imetoa ithibati ya aina 22 za vitabu vya ziada vya mitaala iliyoboreshwa, mtaala unaoendelea vitabu 156 na maudhui 18 ya kielektroniki;
  • imetoa ithibati kwa miswada ya vitabu 162 kati ya 203 kutoka kwa wachapaji binafsi; na
  • imechapa na kusambaza vitabu vya kiada nakala 2,687,860 vya sekondari vya masomo ya sayansi na hisabati kidato cha 1 – 4; nakala 4,776,461 za vitabu vya darasa la IV – VII; na nakala 4,000,000 za vitabu vya hadithi kwa elimu ya awali, darasa I na II, 6,060 za vitabu vya breli kwa ajili ya wanafunzi wa awali. Aidha, vitabu vyote vilivyochapwa na kusambazwa vinapatikana pia katika maktaba mtandao ambapo wanafunzi na walimu wanaweza kuvipata bila gharama yoyote ya kuunganishwa kwa mtandao (Zero – Rating) na hivyo kurahisisha upatikanaji wake.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kukuza ujuzi wa uandishi, kuhamasisha tabia ya usomaji na kuongeza machapisho katika maktaba zetu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imefanya Maadhimisho ya Wiki ya Usomaji Vitabu Mkoani Mwanza ikiwa na kauli mbiu ‘Wasomaji na Wachapishaji Tukutane Maktaba’, lengo ni kuhamasisha jamii kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu;
  • imeratibu mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi 442 wa shule za sekondari ambapo washindi watano walipatikana kwa ajili ya kushiriki mashindano ngazi ya kikanda. Lengo la mashindano hayo ni kukuza stadi na ujuzi wa uandishi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini;
  • imeratibu utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Unaozingatia Ubunifu uliofanyika tarehe 13 Aprili, 2024 ambapo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Prof. Abdulrazak Gurnah ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Nobel katika fasihi kwa mwaka 2021. Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Unaozingatia Ubunifu imehusisha mashindano ya uandishi wa riwaya, mashairi na hadithi za watoto ambapo jumla ya miswada 208 (Riwaya 51, Ushairi 97 na Hadithi za watoto 60) ilipokelewa ambapo washindi 10 kutoka katika kila nyanja walitunukiwa cheti kila mmoja. Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alipata ngao pamoja na fedha tasilimu wakati mshindi wa pili na wa tatu walipata zawadi ya fedha tasilimu pekee.  Lengo la Tuzo hiyo ni kuhamasisha uandishi utakaosaidia kuongeza idadi ya vitabu vilivyoandikwa na Watanzania na kutumika katika shule zetu badala ya kutegemea vitabu vinavyotoka nje ya nchi; na
  • imeendelea kuimarisha fursa za huduma ya maktaba nchini kwa kuendelea na ujenzi wa maktaba ya Kumbukumbu ya John Pombe Magufuli – Chato. Vilevile, imetoa mafunzo ya muda mfupi kwa wakutubi 70 wa maktaba kuhusu huduma za maktaba na matumizi ya mfumo wa malipo ya Serikali. Aidha, imepokea nakala za vitabu 62,777 kutoka katika taasisi mbalimbali za kielimu na kusambaza katika maktaba zetu.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha fursa na ubora wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuondoa vikwazo katika ufundishaji na ujifunzaji, Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imekamilisha Kiunzi cha Kitaifa cha Kuwezesha Shule zinakuwa Jumuishi zaidi (National Framework for Enabling Schools to Become More Inclusive). Kiunzi hicho kimebainisha vigezo vya shule kuwa jumuishi na namna ya kuvifikia vigezo hivyo;
  • imesambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa saidizi kwa ajili ya wanafunzi, wakufunzi, walimu na walimu tarajali wenye mahitaji maalum katika shule za msingi 732, vitengo 565 na shule jumuishi za sekondari 72. Vifaa hivyo ni pamoja na: Hansonet 60, Shimesikio 79, fimbo nyeupe 62, Orbit Reader 107, miwani za jua 52, magongo 29, mashine za breli zinazotumia umeme 17, vitimwendo 120, vioo-kuza vinavyotumia umeme (Electronic Magnifier) 25, kofia 43, karatasi za kuandikia maandishi ya breli box 119 na seika 89 kwa walimu wasioona kwa lengo la kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji wa elimu maalum; na
  • imewezesha zoezi la upimaji kwa wanafunzi 935 viziwi na kubaini wanafunzi 281 wenye usikivu hafifu ambao walipatiwa hearing aids, wanafunzi 300 wenye maambukizi walishauriwa kwenda hospitali na wanafunzi 354 viziwi kabisa walipewa tablets zenye kamusi ya lugha ya alama.
  • Mheshimiwa Spika, katika eneo la upimaji na tathmini ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu, Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imeendesha Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) wa mwaka 2023 kwa wanafunzi 1,545,330 ambao ni sawa na asilimia 91.25 ya wanafunzi 1,693,444 waliosajiliwa. Katika upimaji huo wanafunzi 1,287,934 sawa na asilimia 83.34 walifaulu;
  • imeendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi wa mwaka 2023 kwa watahiniwa 1,356,392 ambao ni sawa na asilimia 97.07 kati ya 1,397,293 waliosajiliwa. Katika mtihani huo wanafunzi 1,092,960 sawa na asilimia 80.58 walifaulu;
  • imeendesha Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili wa mwaka 2023 kwa wanafunzi 695,639 ambao ni sawa na asilimia 91.56 kati ya 759,799 waliosajiliwa. Katika upimaji huo wanafunzi 592,741  sawa na asilimia 85.31 walifaulu;
  • imeendesha Mtihani wa Kidato cha Nne wa mwaka 2023 kwa watahiniwa 529,596 ambao ni sawa na asilimia 97.47 kati ya 543,332 waliosajiliwa. Katika mtihani huo wanafunzi 471,427 sawa na asilimia 89.36 walifaulu;
  • imeendesha Mtihani wa Maarifa kwa watahiniwa 8,630 kati ya watahiniwa 10,953 waliosajiliwa kufanya mtihani ambapo watahiniwa 4,239 sawa na asilimia 49.12 walifaulu; na
  • imesajili watahiniwa 104,172 kwa ajili ya Mtihani wa Kidato cha Sita ambao umeanza kufanyika tarehe 6 Mei, 2024 na watahiniwa 11,534 wa Mtihani wa Ualimu.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha elimu inayotolewa katika vituo vinavyotoa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imesajili wanafunzi 22,131 wakiwemo wasichana 2,794 wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala katika vituo vya elimu ya Watu Wazima. Vilevile, imetoa mafunzo ya kisomo kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa watu wazima 6,238 katika mikoa 26;
  • imekamilisha moduli 11 za Hatua ya I na II kwa ajili ya vituo 151 vya elimu ya sekondari kwa Njia Mbadala ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika vituo hivyo; na
  • imeongeza idadi ya vituo vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala kutoka 168 hadi kufikia 190 kwa lengo la kuongeza fursa kwa wanafunzi waliokosa elimu kwa sababu mbalimbali.


d.   Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Juu

  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kupitia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imetoa mikopo kwa wanafunzi 229,652 (mwaka wa kwanza 83,640 na wanaoendelea 146,012) yenye jumla ya Shilingi 786,724,730,000.00;
  • imetoa ufadhili kwa wanafunzi 1,220 kati ya 1,200 waliolengwa (wanafunzi wapya 915 na wanaoendelea 305) wenye jumla ya Shilingi 6,367,169,632.00 kupitia SAMIA Scholarship;
  • imetoa mikopo kwa wanafunzi 2,299 wa ngazi ya stashahada yenye jumla ya Shilingi 6,114,790,500.00; na
  • imekusanya jumla ya Shilingi 132,731,358,063.47 sawa na asilima 55 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 241 kutokana na mikopo iliyoiva.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ithibati na uthibiti wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeratibu maombi 144,755 ya wanafunzi walioomba kujiunga na elimu ya juu kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika vyuo vikuu nchini kwa mwaka wa masomo 2023/24. Kati ya maombi hayo, waombaji 133,617 sawa na asilimia 92 wamedahiliwa katika vyuo mbalimbali nchini;
  • imefanya tathmini na kutoa ithibati ya Mitaala 65 kati ya mitaala 289 iliyopokelewa kwa mchanganuo ufuatao: Ngazi ya astashahada 3, stashahada 3, shahada 20, stashahada ya uzamili 2, uzamili 34 na uzamivu 3; na
  • imetathmini na kutambua tuzo 2,076 sawa na asilimia 83 ya tuzo 2,515 zilizowasilishwa kutoka vyuo vya elimu ya juu vya nje ya nchi.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu na kuongeza fursa katika vyuo vikuu na taasisi za sayansi na teknolojia kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeendelea na taratibu za ujenzi wa miundombinu katika Kampasi 14 za vyuo vikuu ambapo ujenzi katika Chuo Kikuu Ardhi umefikia asilimia 48, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kampasi kuu asilimia 35, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kampasi ya Rukwa asilimia 45 na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwl. Julius Nyerere kampasi kuu asilimia 15; Aidha, zoezi la kupata wakandarasi katika kampasi zilizobakia linaendelea; na
  • inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika vyuo vikuu ikiwemo kumbi za mihadhara, hosteli za wanafunzi, madarasa na maabara.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za sayansi na teknolojia kwa kuwawezesha jumla ya wanafunzi 3,107 (wanafunzi 517 kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na wanafunzi 2,590 kutoka chuo cha Ufundi Arusha) kuhudhuria mafunzo ya vitendo kwenye viwanda, kampuni na taasisi mbalimbali nchini. Vilevile, imetoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi 1,966 wa “cluster” ya pili na ya tatu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea uwezo wahadhiri na watumishi waliopo katika taasisi za elimu ya juu, Serikali imewezesha mafunzo ya muda mrefu kwa wanataaluma 396 (umahiri 189 na uzamivu 207) kutoka vyuo vya elimu ya juu wakiwemo wanataaluma 27 kutoka vyuo binafsi. Vilevile, imewezesha mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 24 (shahada 9, stashahada 14 na astashahada 1). Aidha, imewezesha mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 1,557.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi za nje na vyuo vikuu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeratibu ufadhili wa wanafunzi 23 wanaosoma nchini China kupitia programu ya China Scholarship Council. Vilevile, imeendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi watano wa kutoka China wanaosoma Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na
  • imefadhili wanafunzi 193 katika programu mbalimbali kupitia Jumuiya ya Madola ya Uingereza 9, Chevening UK 17, Hungary 23,Urusi 90,Mauritius2 naChina 52.


e.   Kuimarisha Uwezo wa Nchi Katika Tafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Lengo la Kuchochea Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda

  • Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeendelea kuimarisha tafiti kwa lengo la kutumika kutatua changamoto mbalimbali za jamii na kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeendelea kuratibu miradi 106 ya utafiti na ubunifu kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia – COSTECH ikiwemo miradi 34 ya utafiti na miradi 72 ya ubunifu katika vyuo vikuu, taasisi za maendeleo pamoja na vyuo vya kati vya ufundi ambapo miradi saba imekamilika na kufungwa. Utekelezaji wa miradi hiyo umewezesha upatikanaji wa bidhaa, teknolojia na kampuni changa. Kwa mfano, kampuni nne zimezalishwa na kusajiliwa kutoka katika miradi hiyo ya ubunifu na kuajiri vijana 27;
  • imefanya tafiti 638 kupitia taasisi za elimu ya juu katika maeneo ya elimu, afya, mazingira, uongozi, viwanda, TEHAMA, usafirishaji, kilimo, ubunifu, kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia taka zinazozalishwa katika mazingira ya nyumbani, tiba za wanyama, biashara, haki za binadamu, watu wenye mahitaji maalum, matumizi bora ya ardhi, usanifu na ujenzi wa gharama nafuu wa majengo mapya, njia mbadala za uvunaji wa maji ya mvua; na
  • imeendelea kusimamia miradi ya tafiti 199 katika maeneo yafuatayo: utatuzi wa migogoro ya ardhi, matumizi bora ya ardhi, usanifu na ujenzi wa gharama nafuu za majengo mapya, njia mbadala za uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza huduma ya maji katika majiji, ubunifu na matumizi ya maeneo ya wazi katika kuzuia mafuriko, kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia taka zinazozalishwa katika mazingira ya nyumbani na uzalishaji wa chakula kwa kutumia skimu ndogo ndogo za maji katika vijiji vilivyokaribu na mito.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imeandaa andiko mradi la kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Teknolojia (National Technology Park), kuandaa dira ya miaka 15 ya mahitaji ya teknolojia nchini (National Technology Roadmap);
  • imeboresha vyuo vya maendeleo ya wananchi 12 ili vitumike katika kuchagiza uibuaji na uendelezaji wa bunifu na teknolojia (Upgrading 12 FDCs into Zonal/Regional Innovation and Technology Support Centers);
  • imeandaa andiko mradi la kuanzisha vituo vinne vya umahiri wa utafiti na ubunifu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela. Aidha, vituo hivyo vitajikita katika Teknolojia zinazoibukia (Emerging Technologies); Bidhaa na Maarifa Asilia (Natural Products and Indigenous Knowledge); Sayansi na Teknolojia za Anga (Space Science and Technologies); Chanjo na Teknolojia za kubaini magonjwa ya binadamu na wanyama (Vaccine and Diagnostics for Human and Animal Diseases); na Teknolojia za kufundishia na kujifunzia yaani (Educational Technologies); na
  • imetoa tuzo za watafiti kwa washindi 47 waliochapisha matokeo ya tafiti katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia taasisi za elimu ya juu imetoa machapisho 1,519 kati ya machapisho 1,806 yaliyolengwa katika majarida mbalimbali ya kitaaluma kwenye ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa lengo la kuongeza maarifa katika jamii kuhusu utatuzi wa changamoto mbalimbali na kuvitangaza vyuo. Vilevile, imefadhili wanataaluma 173 ili kufikia hatua ya kuchapisha machapisho katika majarida mbalimbali.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu, Serikali imetekeleza yafuatayo:
  • imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyingine za kufundishia na kujifunzia kwa lengo kuongeza ufanisi katika ufundishaji;
  • imeendelea kusimamia bunifu mbalimbali zilizobuniwa kupitia watumishi na wanafunzi ili ziweze kufika hatua ya kuuzika sokoni, bunifu hizo ni uundaji wa mita za malipo kabla ya matumizi; Programu ya Bi – Shamba na Programu ya Leo Leo Gulio;
  • imewezesha taasisi iitwayo UjuziNet kutengeneza programu ya simu kwa ajili ya kutafuta taarifa za teknolojia. Programu hiyo itaziwezesha taasisi za umma na binafsi kukusanya taarifa kuhusu Teknolojia zinazopatikana katika sekta mbalimbali. Programu hii imeundwa mahsusi ili kunasa taarifa katika umwagiliaji wa kilimo, taarifa za teknolojia ya afya, na mitambo ya kilimo, kulingana na mahitaji yaliyopokelewa; na
  • imewezesha ubiasharishwaji wa bunifu nne (ushonaji, ubunifu wa mavazi, mashine za kuongeza madini joto kwenye chumvi na mashine ya kufungasha bidhaa mbalimbali) katika Kanda ya Dar es Salaam kupitia VETA.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia taasisi za elimu ya juu imeendelea kuimarisha huduma za jamii na kutatua changamoto mbalimbali, kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imetoa ushauri wa kitaalamu katika usanifu na usimamizi wa ujenzi wa ghorofa tatu wa jengo la ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba – TMDA Dodoma; usanifu na usimamizi wa ujenzi wa uwanja wa mashujaa (National Heroes Stadium) katika mji wa Serikali Dodoma; usanifu na usimamizi wa ukarabati wa majengo ya biashara, nyumba ya ukewezaji, maisha house, NIC Kisutu, NIC Morogoro na Kihonda apartments. usanifu na usimamizi wa ujenzi wa karakana za TEMESA katika mji wa Dodoma na Geita kupitia VETA; na
  • imetoa ushauri kwa wadau mbalimbali ikiwemo huduma za ugani kwa washiriki wapatao 65,306 wakiwemo wakulima, wafugaji, maafisa ugani, watafiti katika nyanja ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na uimara wa udongo.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti na kukuza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa kutekeleza yafuatayo:
  • imesajili vituo vipya 43 vya Mionzi ayonishi na kufikisha jumla ya vituo vya mionzi 1,386 vilivyosajiliwa na vituo vipya 42 vya mionzi isiyoayonishi na kufikisha jumla ya vituo vya mionzi isiyoayonishi 409 vilivyosajiliwa. Aidha, imesajili vyanzo vipya 36 vya mionzi na kufikia jumla ya vyanzo vya mionzi 1,647 vilivyosajiliwa;
  • imetoa leseni 633 za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi, uingizaji nchini wa vyanzo vya mionzi 95, utoaji nje ya nchi wa vyanzo vya mionzi 13 na safirishaji wa vyanzo vya mionzi ndani ya nchi 47;
  • imepima viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 1,980 wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi katika vituo 429. Aidha, viwango vya mfiduo vilivyopokelewa katika miezi mitatu mfululizo vilianzia 0.1 hadi 3.2 millisievert (mSv), ambavyo viko ndani ya ukomo unaokubalika wa udhibiti;
  • imepima sampuli 37,717 za vyakula na mbolea, kati ya sampuli hizo 9,062 ziliingia nchini, sampuli 27,774 zilisafirishwa nje ya nchi na sampuli 695 zilikuwa za mbolea na tumbaku na bidhaa nyingine. Upimaji ulibaini kuwa sampuli hizo hazikuwa na madhara yoyote yatokanayo na mionzi; na
  • imeanzisha ofisi kwenye Bandari ya Fumba Unguja kwa ajili ya usimamizi wa usalama na udhibiti wa vyanzo vya mionzi ayonishi (ionizing radiation) na mionzi siyoayonishi (non ionizing) kwa ajili ya ulinzi wa umma.


D.  TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

  • imewajengea uelewa wadau kwa kutoa mafunzo kuhusu umuhimu wa Tanzania kuridhia Mkataba wa 2001 wa Urithi wa Chini ya Bahari (Underwater Heritage) uliokuwa na lengo la kulinda urithi wa kiutamaduni hususan kumbukizi za binadamu zenye sifa ya kiutamaduni, kihistoria na kiikolojia; na
  • imehamasisha matumizi ya mitandao ya UNESCO (ASPNet, UNEVOC, UNITWIN) kwa wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu kwa lengo la kubadilishana taarifa za kitaaluma, kuongeza maarifa na utendaji katika maeneo ya umahiri. Aidha, mpaka sasa taasisi 10 zimejiunga na Mtandao wa ASPnet na taasisi nne na vyuo vikuu viwili vimejiunga na mtandao wa UNITWIN/UNESCO Chairs.


MWELEKEO WA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25 KWA FUNGU 46

  • Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika. Vilevile, vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.
  • Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kama vifuatavyo:
  • kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini;
  • kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu);
  • kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu;
  • kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu; na
  • kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.


  1. Kuendelea na utekelezaji wa Sera na Mitaala, Mapitio ya Sheria  na kuandaa Miongozo ya Utoaji Elimu na Mafunzo Nchini
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu. Aidha, itaendelea na uandaaji wa zana za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 ambazo ni Miongozo, Mfumo wa Kitaifa wa Tuzo na Sifa Linganifu (Tanzania Qualification Framework – TQF), Sheria na Kanuni, Mfumo wa Mtaala wa Kitaifa na Mfumo wa Tathmini wa Kitaifa katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari, Ualimu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Juu kwa lengo la kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Sera.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na maboresho ya mitaala ya elimu ya amali sanifu na elimu ya juu ili kuwezesha nchi kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu. Aidha, itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimaliwatu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi;
  • itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu; na
  • itahakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kwa watendaji wa ngazi zote za elimu na mafunzo wakiwemo walimu wa shule za msingi; walimu wa shule za sekondari; wakufunzi wa vyuo vya ualimu; wakufunzi wa vyuo vya ufundi; wakufunzi wa vyuo vya VETA; wakufunzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi; maafisa elimu msingi, maafisa elimu sekondari, wasimamizi wa elimu ngazi ya mkoa; maafisa elimu kata; wathibiti ubora wa shule; na wanataaluma kutoka taasisi za elimu ya juu. Vilevile,itaendelea kutoa mafunzo kazini kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kuhusu mitaala iliyoboreshwa.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura 353 ili iendane na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023. Vilevile, itafanya mapitio ya sharia na miundo ya taasisi mbalimbali ikiwamo; COSTECH, TLSB, NECTA, VETA, TCU, NACTVET, TIE, TEWW na TEA ili ziendane na maboresho ya Sera na Sheria na makuliano mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa. Vilevile, itafanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kuongeza ufasini wake ikiwamo kurahisisha ufunguaji wa mashauri na utekelezaji wake.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhuisha miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na maboresho ya Mitaala na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 kama ifuatavyo:
  • itakamilisha Mwongozo wa Kuwatambua na Kuwaendeleza Wanafunzi wenye Vipawa na Vipaji; na
  • itaandaa Mwongozo wa Elimu Jumuishi wa Ufundishaji na Matumizi ya Teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaongeza wigo wa ukusanyaji, uchakataji na utoaji wa takwimu za elimu kwa kuunganisha mifumo yote ya takwimu za elimu ya awali, msingi, sekondari, ualimu, ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, elimu ya juu, pamoja na mifumo ya upimaji na tathmini. Maboresho hayo yatahusisha kujumuisha taarifa za shule binafsi zisizo tumia mitaala ya Taifa. Mabadiliko hayo yatawezesha Wizara kuwa na taarifa za kila mwanafunzi, fani na programu zinazotolewa nchini na kuandaa Kitabu cha Taifa cha Takwimu Muhimu za Elimu (Basic Education Statistics in Tanzania – BEST) ambacho kitakuwa na taarifa za kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu. Kazi ya maboresha hayo imeshaanza na inafanywa na wataalamu wa ndani kutoka vyuo vikuu. Aidha, Serikali itaanzisha jukwaa shirikishi la utafiti la wadau wa elimu ambalo litatambua na kuratibu tafiti za kielimu zinazofanyika nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa maamuzi ya kimageuzi na maendeleo katika sekta yanazingatia taarifa, takwimu na tafiti sahihi zenye maslahi kwa sekta na Taifa kwa ujumla.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha tunaimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo, Serikali itaendelea na mapitio ya Sera ya Sayansi na Teknolojia ya Mwaka 1996 kwa lengo la kuandaa sera inayoakisi hali ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.


  • Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Mafunzo ya Amali (Ufundi na Ufundi Stadi) katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Amali.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na sekondari za amali ili kuongeza fursa za mafunzo kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itawezesha ujenzi wa shule mpya za sekondari za amali za uhandisi 100 kati ya hizo shule 26 zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2025. Aidha, ujenzi wa shule za amali utapewa kipaumbele katika maeneo ambayo hayana vyuo ya mafunzo ya ufundi stadi;
  • itaendelea na ujenzi wa vyuo 65 vya mafunzo ya ufundi stadi, kati ya hivyo 64 ni vya wilaya na kimoja ni cha ngazi ya Mkoa wa Songwe. Vilevile, imeongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo 29 vilivyokamilisha ujenzi;
  • itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya nyongeza katika vyuo 10 vya mafunzo ya ufundi stadi (Ndolage-Muleba, Ileje, Newala, Ngorongoro, Gorowa – Babati, Urambo, Kasulu, Mabalanga – Kilindi, Nkasi na Kanadi – Bariadi) ili kuviwezesha vyuo hivyo kufikia viwango vya msingi vya utoaji wa mafunzo; na
  • itaendelea na ujenzi wa hosteli mbili katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 768 kwa kila hosteli. Vilevile, itaendelea na ujenzi wa maktaba yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,500, ukumbi wa mihadhara utakaohudumia wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja na itajenga madarasa 12 yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 300 kwa kila darasa na ofisi 20 za watumishi katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Kivukoni. Aidha, itaendelea na ujenzi wa jengo la utawala na madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,800 katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Pemba. Aidha, itaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza fursa za mafunzo ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itasajili vyuo vya elimu ya ufundi  na mafunzo ya ufundi stadi 150 ambapo vyuo vya elimu ya ufundi ni 100 na vyuo  vyamafunzo ya ufundi stadi ni 50,hivyo kuwa na jumla ya vyuo 504 vya elimu ya ufundi na vyuo 885 vya mafunzo ya ufundi stadi. Usajili wa taasisi hizo utawezesha kuongeza fursa na kutoa mafunzo kwa kuzingatia viwango na ubora;
  • itadahili wanafunzi 263,718 wa elimu ya ufundi na mafunzo na ufundi stadi ambapo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi ni 190,518 na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200 sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na udahili wa mwaka 2023/24. Udahili unalenga kuongeza rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa;
  • itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini ikiwamo fani sayansi na ufundi; na
  • itadahili wanafunzi 2,089 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC ili kuongeza idadi ya walimu wanaofundisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya ualimu wa mafunzo ya ufundi.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea umahiri walimu wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na vyuo vya maendeleo ya wananchi, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itatoa mafunzo kwa walimu 1,000 wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuhusu tathmini ya mitaala ya umahiri ili kuwawezesha walimu kufundisha na kufanya tathmini ya wanafunzi kwa kuzingatia umahiri; na
  • kuendelea kuboresha vituo vya umahiri kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa mafunzo wa fani za kipaumbele kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.
  • Kuwezesha Ongezeko la Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu
  • Mheshimiwa Spika, katika kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itawezesha ujenzi wa shule za sekondari za kata 226, nyumba za walimu 184 wa sekondari na ununuzi wa vifaa vya maabara;
  • itawezesha ujenzi wa madarasa 2,018 (msingi 1,221 na sekondari 797); mabweni 114 kwa shule za sekondari; nyumba za walimu 658 (msingi 567 na sekondari 81) matundu ya vyoo 2,848 (msingi 1,514 na sekondari 884), maabara 10 na vituo vya walimu (TRCs) 300 kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, itakamilisha ujenzi vyumba vya madarasa 111 katika shule za msingi 37, matundu ya vyoo, maabara, nyumba za walimu na mabweni katika shule za sekondari 50; na
  • itaweka nishati safi ya kupikia ili kuendelea kuhifadhi na kuimarisha mazingira katika vyuo vya ualimu 11 (Nachingwea, Katoke, Kleruu, Tabora, Dakawa, Patandi, Mpwapwa, Sumbawanga, Mhonda, Kasulu na Monduli). Vilevile, itanunua samani kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda, Dakawa na Ngorongoro.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa ithibati kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itasajili shule za msingi na sekondari takribani 772 ambapo awali pekee 30, awali na msingi 475 (zisizo za Serikali 162), sekondari 266 (zisizo za Serikali 57), chuo cha ualimu kimoja cha binafsi; na
  • itafanya tathmini kwa shule 100 zilizopewa usajili wa masharti ili kubaini utekelezaji wa masharti ya usajili.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uthibiti ubora wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na vyuo vya maendeleo ya wananchi, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itafanya tathmini ya jumla katika asasi 6,620 (shule za awali na msingi 4,965, sekondari 1,525, vyuo vya ualimu 66, vyuo vya maendeleo ya wananchi 14, na vituo 50 vya elimu ya watu wazima na mafunzo nje ya mfumo rasmi). Vilevile, itafanya ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kubaini ubora katika uandikishaji, ufundishaji na ujifunzaji, usimamizi na uongozi na kutoa ushauri kwa walimu wa masomo katika taasisi 1,010;
  • itaendelea na ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na ukarabati wa ofisi nne za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mpwapwa, Chato, Mpanda, na Halmashauri ya Mji – Ifakara;na
  • itanunua samani na vitendea kazi katika ofisi 210 (halmashauri 184 na mikoa 26) za uthibiti ubora wa shule na itanunua magari 3 kwa ajili ya shughuli za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mlele, Tunduma na Serengeti.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kuimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi na hivyo kuboresha ufundishaji na ujifunzaji na kuchochea tabia na utamaduni wa kujisomea kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itachapa na kusambaza nakala za vitabu 2,000,000 vya masomo ya Hisabati na Sayansi kwa kidato cha 1 hadi 4;
  • itaandaa vitabu vya kiada kwa darasa la II na IV, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu. aidha, itaweka maudhui ya elimu ya sekondari katika mfumo wa kidijiti kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake;
  • itachapa na kusambaza vitabu vya kiada kwa darasa la ii na iv, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu; na
  • itachapa na kusambaza vitabu vya kiada katika maandishi yaliyokuzwa na breli kwa darasa la II na IV, sekondari kidato cha 1 na cha 6 na viongozi vya mwalimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wenyemahitaji maalum.
  • Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi na kuhamasisha tabia ya usomaji na kuimarisha matumizi ya maktaba katika ngazi zote za elimu kwa kutekeleza yafuatayo: ilevile, Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi na kuhamasisha tabia ya usomaji na kuimarisha matumizi ya maktaba kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itaandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Huduma za Maktaba nchini. Vilevile, itaendelea kununua vitabu kwa ajili ya maktaba za mkoa na kuendeleza Maktaba 15 za Jamii;
  • itaendelea kusimamia na kuratibu utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu yenye lengo la kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu, kutunza historia na utamaduni wa Mtanzania na kuinua sekta ya uchapaji nchini. Tuzo hizo zitatolewa kwa waandishi mahiri wa riwaya, hadithi fupi na ushairi;
  • itagharamia uchapaji, kununua na kusambaza katika taasisi za elimu na maktaba vitabu vya washindi wa tuzo hizo. Mafanikio katika azma hii yamelenga kuwezesha sekta ya uchapishaji na uchapaji na kuongeza ari ya kusoma; na
  • itaendelea kuratibu na kukuza stadi na ujuzi wa uandishi insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini katika nyanja za: ujenzi wa taifa, mageuzi ya kimaendeleo, ustahimilivu, na maridhiano. Tutaandaa shindano maalum la uandishi wa insha kwa wanafunzi kuchochea uelewa na fikra tunduizi kuhusu falsafa ya 4Rs ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, Serikali itaendelea kuratibu shindano la uandishi wa insha kwa Nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa wanafunzi 2,000 wa shule za sekondari.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itanunua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari 1,322 na vyuo 13 vya ualimu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo 35 vya ualimu. Vilevile, itanunua vifaa vya kujifunzia na kemikali kwa ajili ya kufundishia masomo ya sayansi kwa wanafunzi wa elimu kwa njia mbadala kwa hatua ya I na II.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaimarisha utoaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi na walimu wenye mahitaji maalum kwa lengo la kuondoa vikwazo vya kimfumo na kimuundo ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itafanya tathmini ya awali ya kubaini hali ya usaidizi uliopo na unaohitajika kwa wanafunzi 1,000 na walimu 200 wenye mahitaji maalum kwa lengo la kutoa ushauri wa kitaalam;
  • itajenga uelewa kwa jamii na wadau wa elimu kuhusu elimu jumuishi kwa lengo la kuhamasisha uandikishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum;
  • itawajengea uwezo maafisa 368 wa elimu maalum msingi na sekondari kuhusu ubainishaji wa awali wa watoto wenye ulemavu kwa lengo la kurahisisha zoezi la upimaji kwa kiwango kinachohitajika; na
  • itanunua na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa saidizi kwa wakufunzi 105, walimu 103 na walimu tarajali 188 wenye mahitaji maalum ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kufanya upimaji na tathimini ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itaendesha Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili kwa watahiniwa 1,681,490 na 882,314 mtawalia wanaotarajiwa kufanya upimaji huo mwezi Novemba, 2024;
  • itaendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,241,291 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Septemba, 2024;
  • itaendesha Mtihani wa Kidato cha Nne na Mtihani wa Maarifa kwa watahiniwa 559,646 wanaotarajiwa kufanya mitihani hiyo mwezi Novemba, 2024;
  • itaendesha Mtihani wa Kidato cha Sita kwa watahiniwa 114,500 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2025; na
  • itaendesha Mtihani wa Cheti na Stashahada ya Ualimu kwa watahiniwa 8,500 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2025.


  • Kuongeza Fursa na Kuimarisha  Ubora wa Elimu ya Juu
  • Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji, Serikali itatekeleza yafuatayo:
  • itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 223,201 hadi 252,245;
  • itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na SAMIA Skolashipu 2,000. Aidha, itatoa mikopo kwa wanafunzi 157,745 wanaoendelea na masomo;
  • itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
  • itaendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Shilingi Bilioni 198 kutoka sekta ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi. Aidha, itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika wapya 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi; na
  • itaanza kutoa ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwemo eneo la fani ya mionzi na nyuklia.


  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa ithibati na uthibiti wa ubora wa elimu katika ngazi ya elimu ya juu kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itaendelea kuratibu udahili wa wanafunzi 145,800 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kujiunga na programu mbalimbali za masomo katika vyuo vya elimu ya juu; na
  • itafanya tathmini ya maombi ya utambuzi wa tuzo 5,000 za wahitimu  zilizotolewa katika vyuo vikuu vya nje na kuzitambua zitakazokidhi vigezo.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya taasisi za elimu ya juu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itajenga miundombinu katika taasisi za elimu ya juu kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa ajili ya Mabadiliko ya Kiuchumi kama ifuatavyo: kumbi 27 za mihadhara; ofisi 302; vyumba 90 vya madarasa na vyumba 17 vya semina. miundombinu hiyo itajengwa katika kampasi 15 za vyuo vikuu katika mikoa  ifuatayo: UDSM (Kagera, Lindi na Zanzibar); MUHAS (Kigoma); ARU (Sengerema-Mwanza); SUA (Katavi); Mzumbe (Tanga); MUST (Rukwa); UDOM (Njombe); MoCU – (Shinyanga); IAA (Manyara na Ruvuma); TIA (Singida); IFM (Simiyu). Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia Kampasi Kuu Butiama ambapo chuo hicho kitajenga kampasi yake mkoani Tabora; na
  • itaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika taasisi za elimu ya juu ikiwemo ujenzi wa maabara, madarasa na hosteli.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza idadi ya wanataaluma wenye sifa na kuwajengea uwezo watumishi wasio wanataaluma katika taasisi za elimu ya juu ambapo itagharamia mafunzo kwa wanataaluma 308 na watumishi wasio wanataaluma 23 kwa ngazi ya umahiri na shahada ya uzamivu katika fani mbalimbali.
  • Kuimarisha Uwezo wa Nchi katika Utafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili Kuchochea Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaweka mazingira wezeshi kwa kuboresha mifumo ya TEHAMA inayounganisha taasisi za maendeleo ya tafiti, taasisi za elimu ya juu na mifumo ya uratibu wa utafiti na ubunifu ili kurahisisha utendaji wa kazi na upatikanaji wa takwimu mbalimbali zinazohusu utafiti, ubunifu na maendeleo. Vilevile, itaunganisha mifumo ya takwimu za elimu na mafunzo nchini kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuimarisha utoaji wa taarifa za elimu na mafunzo.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha taasisi za elimu ya juu na taasisi za kitafiti kuendelea kufanya utafiti wa kimkakati na kuongeza mchango wake katika ajenda ya maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii kwa kutekeleza yafuatayo:
  • itaandaa mikakati ya utekelezaji na usambazaji wa matokeo ya utafiti;
  • itafanya tafiti 301 katika maeneo ya elimu, sayansi, teknolojia, utawala, ardhi, mazingira, mazao ya kilimo, mifugo, sayansi ya jamii, uongozi, biashara, afya, mifugo, misitu na uvuvi kwa lengo la kuongeza maarifa na kutatua changamoto za jamii;
  • itaandaa machapisho 379 ya tafiti katika maeneo ya elimu, ushirika, afya, usimamizi na uendelezaji ardhi, mazingira, makazi na ujenzi, uongozi; na
  • itatoa mafunzo kwa watafiti kuhusu uandaaji na uchapaji wa majarida ya kisayansi ya ndani (Local Peer Review Scientific Journals) na viunzi vya uthibiti.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa tuzo kwa watafiti watakaochapisha tafiti katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa ili kuhamasisha watafiti wa ndani kufanya utafiti na kuchapisha kazi zao katika majarida husika.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali itaanzisha programu itakayowawezesha vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu kuendeleza mawazo ya ubunifu ili yawe biashara au kampuni changa (Talent Pool Program) kwa ajili ya kujiajiri au kuajiriwa. Aidha, itawawezesha vijana 20 wenye vipaji na wabunifu katika masuala ya uhandisi na teknolojia kupitia programu atamizi.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomu itatekeleza yafuatayo:
  • itaendelea kudhibiti matumizi ya mionzi nchini kwa kukagua vituo 900 ikiwemo hospitali, vituo vya afya, migodi, viwanja vya ndege, na viwanda na majengo yenye mashine za kupima mionzi ili kuhakikisha uwepo wa mazingira salama kwa wagonjwa, wafanyakazi na umma kwa ujumla;
  • itapima na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 wanaofanya kazi katika mazingira ya vyanzo vya mionzi katika hospitali, migodini na viwandani ili kuwalinda dhidi ya madhara yatokanayo na vyanzo vya mionzi sehemu za kazi; na
  • itaendelea na upimaji wa sampuli 50,000 za vyakula, mbolea, tumbaku na bidhaa nyingine zinazoingia na kutoka nchini kupitia mipaka ya nchi ikiwemo viwanja vya ndege na bandari pamoja na sampuli za maji ya visima, wasambazaji na wamiliki wa viwanda ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na mionzi.
  • Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utafiti wa tiba za saratani, Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Utafiti cha Tiba za Saratani (Oncology Research Centre) katika Jiji la Arusha ili kuleta tija na ufanisi katika kukabiliana na tatizo la saratani nchini pamoja na kuimarisha utafiti na uchunguzi kwa kutumia teknolojia ya nyuklia.


E.            MWELEKEO WA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

  • Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO, itaendelea kuratibu, kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kimataifa kwa kutekeleza yafuatayo:
  • kuendelea kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao na mikutano ya UNESCO kwa lengo la kutetea maslahi ya nchi;
  • kuratibu na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba na makubaliano ya kimataifa ya UNESCO ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji; na
  • kushirikiana na wadau katika kuhamasisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

F.   SHUKRANI

  • Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa QS. Omary Juma Kipanga (Mb), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ushirikiano anaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu na kufikia malengo ya wizara. Aidha, napenda kumshukuru Katibu Mkuu Profesa Carolyne Ignatius Nombo, Naibu Makatibu Wakuu, Profesa James Epiphan Mdoe na Dkt. Franklin Jasson Rwezimula kwa kunipa ushirikiano. Vilevile, ninaomba kutoa shukrani zangu kwa kamishna wa elimu, wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wote kwa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa juhudi na ufanisi.
  •  Mheshimiwa Spika, pia ninapenda kuwashukuru viongozi wa vyama vya wafanyakazi, walimu, wanafunzi, na wadau wote wa elimu kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wamiliki na mameneja wa shule, vyuo na taasisi binafsi ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kutoa huduma ya elimu na mafunzo nchini.
  • Mheshimiwa Spika, vilevile, ninawashukuru washirika wa maendeleo na wadau wote wa elimu ambao wamechangia kufanikisha utekelezaji wa mipango na miradi ya elimu, sayansi na teknolojia. Naomba kuwatambua baadhi yao kama ifuatavyo: Afrika Kusini, Brazil, Canada, China, Cuba, Ethiopia, Finland, Hangaria, India, Israel, Italia, Japan, Kenya, Korea ya Kusini, Marekani, Mauritius, Misri, Norway, Sweden, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Urusi, Uturuki, Uswisi. Aidha, natambua pia mchango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.
  • Mheshimiwa Spika, napenda pia kushukuru Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa yaliyochangia kufanikisha miradi na programu za Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ni pamoja na: Aga Khan Education Services, Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, British Council, Campaign for Female Education (CAMFED), Christian Social Services Commission (CSSC), Comprehensive Nuclear–Test – Ban Treaty Organisation (CTBTO), Deutscher Akademischer Austauschdienst (DAAD), Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO), Global Partnership for Education (GPE), Human Development Innovation Fund (HDIF), Inter University Council for East Africa (IUCEA), International Atomic Energy Agency (IAEA), Japan International Cooperation Agency (JICA),Jumuiya ya Madola, Karibu Tanzania Organization (KTO), Korea International Cooperation Agency (KOICA), Plan International, Swedish International Development Agency (SIDA), Tanzania Education Network/Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET),Umoja wa Nchi za Ulaya, United Nations Development Programme (UNDP), United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO), United Nations International Children’s Emergency Fund (UNICEF), United States Agency for International Development (USAID),na Water Aid.

G.     MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2024/25

  • Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,965,330,380,000.00 kwa mchanganuo ufuatao:
  • Shilingi 637,287,706,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara ambapo Shilingi 585,225,031,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 52,062,675,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo; na
  • Shilingi 1,328,042,674,000.00 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 1,033,393,669,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 294,649,005,000.00 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
  • Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,882,154,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Mishahara ni Shilingi 1,319,040,000.00 na Matumizi Mengineyo ni Shilingi 1,563,114,000.00.
  • Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba sasa Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Bajeti ya Wizara (Fungu 46 na Fungu 18) yenye jumla ya Shilingi 1,968,212,534,000.00.
  • Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.
  • Mheshimiwa Spika, Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara https://www.moe.go.tz
  • Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *