HOSPITALI ZATAKIWA KUIMARISHA KARAKANA ZA VIFAA TIBA ILI KUSAIDIA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA UHAKIKA

0

Na WAF – Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amewata Waganga Wafawidhi wa Hospitali nchini kuimarisha karakana za vifaa tiba katika hospitali zao ili ziweze kutengeneza vifaa vitavyoharibika na kuhitaji marekebisho.

Dkt. Jingu amesema hayo leo Mei 7, 2024 Jijini Dodoma wakati akipokea vifaa vya hewa tiba ya Oxygen vilivyotolewa na Shirika la Clinton Health Access Initiative (CHAI) ambalo linajishughulisha na masuala ya kutengeneza vifaa tiba katika baadhi ya Hospitali nchini.

Vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo ni pamoja na Handheld Pulse Oximeters, Oxygen analyzers na Oxygen Wall- Flowmeters (Complete sets) ambavyo vitapelekwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Sekoue Toure, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.

Dkt. Jingu amesema ili vifaa hivyo viweze kudumu na kutoa huduma kwa wananchi ni lazima vifanyiwe matengenezo hivyo Hospitali zilizopata vifaa ni ziimarishe karakana ili waweze kutengeneza vifaa tiba hapa hapa nchini.

Aidha, Dkt. Jingu amesema Serikali ya Rais Samia imewekeza kwenye vifaa tiba kuanzia katika Zahanati hadi Hospitali kubwa ambazo zinawawezesha watoa huduma kutoa huduma bora zinazochagizwa na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa.

“Tunajenga uwezo kwa wataalamu wa karakana ili waweze kutengeneza vifaa tiba vilivyo chakavu vinavyohitaji marekebisho sambamba na kutengeneza vifaa vyetu wenyewe, tuna Kanda saba kila Hospitali na kituo wote wana wataalamu wao wa kufanyia matengenezo”. Amesema Dkt. Jingu.

“Ndio maana ndugu zetu wa CHAIi tunawashukuru sio tu kwa vifaa vya hewa tiba mlivyotoa bali vifaa vyote vya uchunguzi ikiwemo X- ray tutengeneze humu humu kwa kuwatumia wataalam wetu waliojengewa uwezo”. Ameongeza Katibu Mkuu huyo.

Dkt. Jingu ameendelea kutoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani sekta binafsi ina umuhimu mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Clinton Health Access Initiative (CHAI) chini Dkt. Esther Mtumbuka amesema Taasisi hiyo ilianzishwa na aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton mwaka 2002 ikiwa na lengo la kushiriki kutoa huduma za Malaria na chanjo kwa muda mrefu.

“Kwenye chanjo tulishirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuleta majokofu yasiyotumia umeme, tuliweza kufanya majaribio ya vifaa vya kupima joto kutokea mbali ambapo tumefanikiwa katika hilo”. Amesema Dkt. Esther.

Amesema vifaa walivyotoa katika Hospitali wanufaika vitasaidia kufuatilia afya za wagonjwa waliokuwa mahututi au upasuaji na changamoto ya upumuaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *