SPIKA DKT. TULIA AITAKA SERIKALI KULIPA MADENI YA VYOMBO VYA HABARI

0

Kuelekea kilele cha siku ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson amezitaka taasisi za Serikali zinazodaiwa na vyombo vya habari kuvilipa kwa wakati ili kuimarisha uchumi katika sekta hiyo na hatimaye waandishi wa habari waweze kutumia uwezo na ujuzi wa kalamu yao katika kuripoti vyema matukio ya mabadiliko ya tabianchi.

Ameyasema hayo Leo Mei 2, 2024 katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari nchini uliofanyika Jijini Dodoma uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi na waandishi wa habari kutoka Mikoa mbalimbali nchini.

Dkt. Tulia amepongeza mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kutatua changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na kuripoti maendeleo yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Nishati na Maji huku akisisitiza kutumia ipasavyo uhuru walionao.

“Tunawategemea waandishi wa habari kuhabarisha umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Uhuru una mipaka, tukisherehekea uhuru wa vyombo vya habari nchini lazima tufike mahali tuone habari ni nini?, tumefika mahali vyombo vya habari kuzungumza habari binafsi ya yule mtangazaji, tunawategemea sana waandishi wa habari ni vyema mkawa makini na kile mnachokiripoti kwani kina uwezo wa kuvuruga amani iliyopo nchini” Amesema Dkt. Tulia.

Pamoja na Mambo mengine amevishauri vyombo vya habari vinavyoripoti habari za Bunge kutumia waandishi wa kudumu wa Bunge kuliko mfumo wanaoutumia wa kuwabadili kwa misimu jambo linalopelekea kukosa waandishi wabobevu wa habari za Bungeni.

Awali Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu wa vyombo vya habari kuzidi kuimarika na kuchochea maendeleo ya Taifa pamoja na ushirikiano wanaoupata Bungeni katika kufanya mabadiliko na kutunga sheria shirikishi.

“Nalishukuru Bunge lako katika mabadiliko ya Sheria, tumetunga kanuni na nina uhakika mpango wa hizi sheria ni shirikishi, Wanahabari mmekuwa kichocheo kikubwa kwa kuimarisha amani na utulivu wa nchi yetu” Amesema Waziri Nnape.

Hata hivyo maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kauli Mbiu isemayo “Uandishi wa Habari Katika Changamoto za Kimazingira”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *