UJENZI WA HOTELI YA KISASA NI KIVUTIO CHA UTALII CHATO
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo, Dkt. Iman Kikoti Amesema hoteli ya nyota tatu inayojengwa wilayani chato katika Kijiji cha lubambagwe ikikamiliki itakuwa ni Moja ya chanzo kikubwa cha mapato kupitia sekta ya utalii.
Amesema kuwa hoteli hiyo ambayo inajengwa chini ya usimamizi madhubuti wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) nisehemu ya kuimarisha utalii Kwa kuongeza sehemu za malazi Kwa ajili ya wageni ambalimbali wanaotembelea Hifadhi zetu hususani watakaotembelea Hifadhi za taifa kisiwa cha Rubondo na Brigi chato zilizopo Kanda ya magharibi
Akizungumza na waandishi wa Habari ambao wanafanya kazi kubwa ya kutangaza Hifadhi zilizopo na vivutio vyake katika eneo la ujenzi wa hoteli hiyo ya nyota tatu hivi karibuni Dkt Kikoti amesema hoteli hiyo pindi itakapo kamilika itafanya wilaya ya Chato kuwa kitovu cha utalii kanda ya ziwa.
“Hoteli ya nyota tatu inayojengwa katika kijiji cha Rubabangwe ni mradi wa kimkakati wa TANAPA na lengo lake ni kukuza utalii kanda ya magharibi hivyo kama mnavyoona mafundi wapo saiti wakiendelea na kazi na sisi watu Wetu kutoka TANAPA wapo hapa kuhakikisha Kila kitu kinakwenda sawa.”Amesema
Nakuongeza kuwa “Hoteli zilizokuwepo katika ukanda huu hazikuwa zinakidhi viwango vya utalii, hivyo basi shirika letu la Taifa TANAPA likaona ni muhimu kuwekeza ili kuvifikia vivutio vya hifadhi hizi,” amesisitiza
Dkt Kikoti amezitaja hifadhi za taifa zinazopatikana kanda ya magaharibi ni pamoja na Burigi Chato, Ibanda Kyerwa, Rumanyika iliyopo Karangwe na Hifadhi ya taifa kisiwa cha Rubondo.
Akizungumzia zaidi hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo Mhifadhi mkuu Dkt Kikoti amesema ni eneo pekee la utalii lenye uwezo wa kustawisha wanyamapori walipo hatarini kutoweka duniani lakini pia ni eneo ambalo lina sokwe mtu ambao bila shaka hawapatikani mahala pengine.
“Sokwe mtu na tembo ni miongoni mwa wanyama walioko hatarini kutoweka duniani ambapo serikali katika hifadhi hii iliwapandikiza miaka 1960. Iliyopita.
“Dunia ya leo imekubwa na uharibifu wa mazingira wanyama hawana uwezo wa kuishi kwenye maeneo yao ya asili, ndio maana unakuta watu wanatengeneza maeneo ya kutunza wanyama nje na maeneo yao ya asili hivyo historia ya Rubondo ya kuwezesha kustawisha wanyama wengi waliopandikizwa inakifanya kisiwa hiki kuwa cha kipekee,” amesema Afande Dkt .Kikoti
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo Ina jumla ya visiwa 12 vinayopatikana ziwa Victoria katika wilaya ya Chato mkoani Geita inasifika kwa utalii wa kuona wanyama hasa sokwe mtu, utalii wa kukamata samaki (spot fishing), kutembea msituni na utalii wa kuona ndege.
Kuhusu wanyama waliopandikizwa katika hifadhi hiyo amesema walipandikizwa sokwe mtu 16, tembo sita, twiga na ndege aina ya kasuku.nakwamba Sokwe mtu waliopandikizwa ndani ya hifadhi hiyo walitoka nchi za Afrika Magharibi ambapo kwa sasa wameongezeka hadi kufikia zaidi ya 60.
“Tuna maeneo mawili yenye sokwe ndani ya msitu wa hifadhi ya Rubondo; tuna sokwe wanaopatikana eneo la upande wa kaskazini na sokwe wanaopatikana upande wa kusini.
Mbali na shughuli ya kuhifadhi visiwa hivyo kama makazi ya wanyamapori pia wanalinda viumbe maji hasa samaki aina ya sangara na sato ambao huzaliana kwa wingi wakiwa hifadhini humo.
Kwa mujibu wa Dkt .Kikoti Amesema asilimia 80 ya hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo imetawaliwa na uoto wa misitu ya ukanda wa chini wa Congo (lower Congolese forest) inayoifanya kuwa ya kipekee ikilinganishwa na hifadhi nyingine zilizopo nchini lakini Licha ya kuwa na msitu wa asili inao wanyama wa kipekee wa asili maarufu statunga ambapo hupatikana katika ukanda wa hifadhi hiyo tu.
Kwaupande wake askari Mhifadhi daraja la pili wa hifadhi hiyo, Lotiken Ngolien anayesimamia kitengo cha kuzowelesha sokwe, amesema kwa upande wa kaskazini wanyama hao wanapatikana eneo la Kasenye, Masekela na Kameana kwa watu wanaotembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kuona sokwe wakifika katika meneo hayo watawaona kwa ukaribu
Naye mhandisi wa hoteli hiyo ya nyota tatu Abdul Kabeza amesema mradi huo umejengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu mashuhuli na kwamba mradi una jumla ya vyumba 30 vya kulala wageni, kumbi nne za mikutano, ambapo kumbi tatu zitatumiwa na wageni wa nje huku mmoja ukitumiwa na wageni wa ndani.
“Kwa nje mradi utakuwa na swimming pool, viwanja vya michezo na eneo kubwa la ufukwe wa ziwa. Ndani ya mradi kutakuwa na maeneo ya michezo ya ndani, maduka ya kisasa, baa na sehemu za kuuza chakula,” amesema Mhandisi Kabeza.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Said Nkumba akizungumzia vikuza utalii katika wilaya ya Chato amesema uwepo wa uwanja wa ndege wa Geita, umehamasisha kukua kwa utalii na kuwa kivutio kizuri kwa wageni.
Pia, amesema uwanja huo mbali na kuifanya chato kuwa na mandhali nzuri pia unasaidia kufikisha wagonjwa wanaoenda hospitali ya Rufaa ya kanda kwa ajili ya matibabu.
“Hata hii hoteli ya nyota tatu inayojengwa na TANAPA mahala ilipo ni kivutio kizuri na Ikikamilika itaongeza mvuto wa ziwa Victoria,” amesema mkuu wa Wilaya Nkumba.