RAIS SAMIA AIPA TANROADS BIL 66 KUANZA UREJESHAJI MIUNDOMBINU YA BARABARA ILIYOHARIBIKA

0

Na Mathias Canal

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 66 kwa ajili ya kuanza urejeshaji wa miundombinu ya barabara zilizoharibika nchini.

Fedha hizo tayari zimegawanywa kwa mameneja wa TANROADS mikoa yote iliyoathirika kwa ajili ya kufanya kazi kwa haraka usiku na mchana ili kurekebisha kadhia zilizozikumbumba barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Akizungumza jana Jijini Arusha mara baada ya kukagua Barabara ya Afrika Mashariki (Arusha bypass) iliyoharibiwa na mvua hizo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mha. Mohamed Besta amesema kuwa kutokana na udharula huo tayari Rais Samia ametoa fedha za matengenezo ya miundiombinu hiyo ambazo zimeshapelekwa katika Mikoa yote Nchini.

Mhandisi Besta amesema kuwa tayari kazi inaendelea katika maeneo yote nchini na fedha hizo zinaratibiwa na vitengo maalumu vya dharula vilivyopo TANROADS pamoja na ofisi za mikoa.

Ameongeza kuwa kutokana na tathimini iliyofanyika mpaka sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 250 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Barabara kuu za Mikoa yote Nchini ambazo zimeharibika vibaya kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.

Amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo kama Kanda ya Ziwa na Nyanda za juu kusini mwa Nchi mvua zimeendelea kunyesha tangu mwezi Oktoba mwaka jana, na sasa unaelekea mwezi wa saba na mvua bado zinaendelea kunyesha.

“Tunamshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ametupatia shilingi bilioni 66 ambazo tumezisambaza katika Mikoa yote ambapo mameneja wote wa Mikoa wamepewa kutokana na hali ya dharura ya Mkoa husika’’ ameeleza

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi Regnald Massawe amesema Mkoa huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kazi hizo za dharura na matengenezo ya kurejesha miundombinu hiyo yanaendelea kufanyika kwa kasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *