AJIRA MPYA KUPELEKWA KWENYE ZAHANATI ZENYE UHABA WA WATUMISHI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema Serikali inatarajia kutoa kipaumbele katika zahanati zilizo na mtumishi mmoja kwa kuongeza idadi ya watumishi katika ajira mpya zitakazotangazwa ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Dugange amesema hayo bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Bukene Mhe. Selemani Zedi alitaka kujua lini Serikali itaongeza Waganga na Wauguzi katika Zahanati za Buhulyu, Luhumbo, Mambali, Ikindwa, Lukuyi, Mbutu na Karitu zilizopo katika jimbo hilo.
“Tayari Rais ametoa kibali cha watumishi katika sekta ya Afya lakini pia watumishi wa sekta nyingine na serikali inatoa ‘commitment’ leo kwamba zahanati hizi ambazo zinamtumishi mmoja mmoja tutahakikisha kwenye ajira hizi ambazo zitafuata tutapeleka watumishi ili waweze kutoa huduma kwa wananchi” amesema Dkt. Dugange
Akifafanua kuhusu changamoto ya watumishi wa Afya Dkt. Dugange amesema “Serikali imeendelea kuajiri wataalamu wa Kada mbalimbali za afya ambapo katika kipindi cha miaka mitatu Serikali imeajiri jumla ya watumishi 18,418 na kuwapangia vituo kote Nchini”.