STAMICO YATAKIWA KUANZISHA MIGODI MIKUBWA YA MADINI

0

Waziri wa Madini  Mhe.Anthony Mavunde amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuweka mikakati madhubuti ya kukuza uwekwzaji wa shirika na kulifanya kuwa kati ya mashirikia makubwa katika sekta ya madini kwa bara la Afrika.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 18,2024 jijini Dodoma katika kikao kilichohusisha Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO na Menejimenti kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mipango Kazi ya Shirika kwa Mwaka wa  2023/2024.

Akizungumza katika hicho, Waziri Mavunde amesema kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini hivyo STAMICO  inatakiwa kuwekeza zaidi katika utafiti wa madini ili kupata taarifa za kina zitakazowezesha ufunguzi wa migodi mikubwa ya madini badala ya kutegemea wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa uwekezaji wa  madini  kwasasa upo katika madini mkakati na madini adimu yanayotumika katika maendeleo ya tekinolojia , hivyo STAMICO ifikirie kufanya uwekezaji mkubwa katika madini ya aina hiyo yakiwemo madini ya kinywe,makaa ya mawe, Helium na madini ya metali.

Akielezea kuhusu Mpango wa Kuwaendeleza Wachimbaji wadogo wa Madini , Waziri Mavunde ameeleza kuwa wizara kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri itaendelea kuwainua wachimbaji wadogo kwa kufanya tafiti ili kubaini maeneo yenye madini na kuwapatia leseni wachimbaji wadogo ili wachimbe bila kubahatisha.

Waziri ameongeza kuwa wizara inaanzisha Programu ya Uchimbaji wenye Tija Endelevu (MBT) yenye lengo la kuwainua wakina mama na vijana wanaojihusisha na uchimbaji madini kwa kuwapatia nyenzo mbalimbali za uchimbaji.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ameitaka STAMICO kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanya tafiti na kuibua maeneo mapya ya uwekezaji pamoja na kutangaza fursa za rasilimali madini zilizopo nchini.

Awali , akifungua kikao Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi STAMICO Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amesema kuwa STAMICO inaendelea kupongeza miradi ya kimkakati ambapo mpaka sasa imefikia miradi nane ukiwemo mradi wa makaa ya mawe Kiwira , Mkaa rafiki , mradi wa uchorongaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji  STAMICO Dkt. Venance Mwase amesema shirika linaendelea kuongeza vyanzo vyake vya mapato ambapo kwasasa makusanyo yanaendelea  kuongezeka kutoka shilingi bilioni 1.3 mpaka bilioni 63 lengo likiwa ifikapo mwezi Julai 2024  shirika lijitegemee kwa asilimia 100.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia Naibu Katibu Mkuu madini Msafiri Mbibo na watendaji kutoka wizara ya madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *