VITUO NANE VYA AFYA VYAJENGWA HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA

0

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya afya nane katika serikali ya awamu ya sita inayolenga kuongeza miundombinu na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akiongelea mafanikio ya miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita kwa waandishi wa habari ofisini kwake jijini hapa.

“Ndugu waandishi wa habari, katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita tumeshuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya afya katika Jiji la Dodoma, tumejenga vituo vya afya nane. Mpaka sasa vituo viwili vimekamilika. Kituo cha Afya Chang’ombe kimekamilika. Mnafahamu eneo la Chang’ombe lina wakazi wengi zaidi ya 40,000 lakini hawakuwa na kituo cha afya. Pia tumekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Nkuhungu. Kama mnavyofahamu mnaokuja Dodoma, eneo lote la Nkuhungu halikuwa na huduma za afya, lakini serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka mitatu mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha tukaanza ujenzi na kukamilisha Kituo cha Afya Nkuhungu” alisema Dkt. Method.

Aliongeza kuwa eneo la Nzuguni vinajengwa vituo vya afya viwili. “Kituo kimoja kinajengwa Ilazo, barabara ya Marthin Luther na kipo hatua za mwisho za umaliziaji. Kituo tayari vifaa tiba vimeshafika na mafunzo kwa watumishi yametolewa na tunategemea mwezi wa Julai, 2024 kianze kufanya kazi. Ni mradi mkubwa ambao umegharimu takribani shilingi bilioni 2.8 kwa hiyo unaweza kuona kwa kiasi gani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi hizo kwa kuwezesha huduma za afya ziwe bora katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Dkt. Method.

Dkt. Method ambae pia ni Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma alisema kuwa serikali inajenga vituo vya afya vinne katika barabara ya mzunguko ‘ring road’. “Ukiangalia kwenye uboreshaji wa miundombinu, mheshimiwa Rais anajenga barabara lakini pia anajenga na vituo vya afya ambavyo vitatoa huduma kwenye hiyo barabara ya mzunguko. Vituo hivyo vitajengwa katika Kata ya Ihumwa, Kata ya Nzuguni eneo la Mahomanyika, Kata ya Nala na Kata ya Makutopora. Kwa hiyo, utaona ni uwekezaji mkubwa sana wa hivi vituo ambavyo vinajengwa. Kwa ujenzi tu wa hivi vituo, kuna wananchi zaidi ya 400,000 wanawenda kunufaika kwa sababu hivi vituo vinajengwa katika maeneo ambayo yanawakazi zaidi ya 50,000 kwenye kata” alisema Dkt. Method.

Akiongelea ujenzi unaoendelea wa vituo viwili vya afya vya Kizota na Zuzu alisema vipo hatua za mwisho kukamilika. “Halmashauri ilipeleka fedha kwa maelekezo ya mheshimiwa Rais kujenga kituo cha Afya Kizota ili kihudumie wananchi wa Kata ya Kizota. Kituo kipo katika hatua za mwisho kukamilika. Pia kuna ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Zuzu, nacho kipo katika hatua za mwisho kabisa kukamilika. Ukiangalia miundombinu hii ambayo inajengwa, utaona ni jinsi gani mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyodhamiria kuliweka Jiji la Dodoma katika mpango mkakati wa kuweza kupokea ongezeko la watu kama makao makuu” alisema Dkt. Method.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *