SILLO AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUTOA BIL. 9.8 UJENZI BARABARA YA LAMI DAREDA MJINI –  DAREDA MISSION BABATI

0

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 9.8 kwa ajili ya Ujenzi wa Barabara ya Dareda Mjini mpaka Dareda Misssion kwa kiwango cha lami.

Mhe. Sillo ametoa shukrani hizo Machi 06, 2024 kwa niaba ya wananchi wa Babati Vijijini na Mkoa wa Manyara kwa ujumla katika hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya nchini China.

“Wananchi wa Babati wamekuwa wakisubiria barabara hiyo kwa hamu sana ambapo ikikamilika itasaidia kukuza uchumi wa wana Babati na Mkoa wa Manyara kutokana na uzalishaji mkubwa wa kilimo unaofanyika na shughuli mbalimbali za kiabiashara” Alisema Mhe. Sillo.

Aidha, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alimuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi wa Kampuni ya Jiangxi Geo Engineering kukamilisha kwa wakati ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Dareda hadi Dongobesh (km 60) sehemu ya kwanza ya Dareda Mjini hadi Dareda Missioni (km 7) ili kuufungua kiuchumi Mkoa wa Manyara.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendinga alieleza kuwa Mradi huo unapita katika Wilaya ya Mbulu na Babati na ujenzi wa barabara utaongeza thamani ya mazao shambani ikiwemo kilimo na ufugaji pia itarahisishia wananchi kufanya biashara pembezoni mwa barabara na kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Mkoa kwa ujumla.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta alisema kuwa, Mkandarasi aliyeshinda zabuni ni kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China, kwa gharama ya Shilingi Billioni 9.88 ambapo utasimamiwa na Wataalamu wa ndani katika kitengo cha Usimamizi (TECU), na kuongeza kuwa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya pili ya Dareda Mission – Dongobesh (Km 53) inatarajiwa kutangazwa Mwaka huu wa fedha 2023/24.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *