MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA KATIKA SEKTA YA UJENZI
Serikali imesema imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wenye jumla ya kilometa 1, 198.50 katika kipindi cha miaka mitatu cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwezi Machi, 2021.
Hayo yamesemwa Aprili 5, 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa hafla ya kuelezea mafanikio ya Sekta ya Ujenzi katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani.
“Katika kipindi cha miaka hii mitatu, barabara 25 zimekamilika na 57 zenye urefu wa kilometa 3,794.11 zinaendelea na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara ya Ujenzi imetenga miradi itakayotekelezwa na wazawa kwa lengo la kuwajengea uwezo makandarasi na Wahandisi Washauri elekezi wa ndani.
“Katika mwaka wa fedha 2023/24 Wizara inatekeleza miradi 12 ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambayo imetengwa mahsusi kwa ajili ya Makandarasi Wazawa ikiwemo barabara ya Monduli – Engaruka – Ngareshi – Enguiki (km 11); Kamsamba – Mlowo (km 147); Changombe – Patamela – Makongolosi (km 30); na Puge – Ziba (km 11)”, amefafanua Bashungwa.
Bashungwa amesema katika kipindi cha miaka mitatu Sekta ya Ujenzi imefanikisha ujenzi wa madaraja makubwa 8 yakiwemo Daraja la Wami mkoani Pwani, Daraja la Tanzanite mkoani Dar es Salaam, Daraja la Gerezani mkoani Dar es Salam, Daraja la Mpwapwa mkoani Dodoma, Daraja la Kiegeya mkoani Morogoro, Daraja la Ruhuhu mkoani Ruvuma, Daraja la Kitengule mkoani Kagera na Daraja la Msingi mkoani Singida.
Vilevile, Bashungwa ameeleza kuwa madaraja matano yapo katika hatua mbalimbali za Utekelezaji ikiwemo Daraja la J.P Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza ambao umefikia 85%, Daraja la Pangani mkoani Tanga umefikia 23%, Daraja la Mbambe mkoani Pwani umefikia 15% na Daraja la Mpiji Chini mkoani Dar es Salaam.
Kuhusu utekelezaji wa Viwanja vya Ndege, Waziri Bashungwa amesema kuwa Sekta ya Ujenzi imekamilisha Viwanja vya Ndege 5 vikiwemo Kiwanja Cha Ndege cha Geita, Mwanza, Mtwara, Songwe na Songea.
Ametaja miradi mingine ya Viwanja vya Ndege ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambayo ni Kiwanja Cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Kiwanja cha Ndege cha Kigoma (Awamu ya tatu), Kiwanja cha Ndege Moshi, Kiwanja cha Musoma, Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga, Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga na Kiwanja cha Ndege cha Tabora (Awamu ya tatu).
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi.